Habari Mseto

Sababu ya Kenya Power kubadilisha jina

October 2nd, 2019 1 min read

Na MARY WANGARI

Ni rasmi sasa! Taasisi ya umma ya Kenya Power and Lighting Company Limited ina jina jipya.

Hii ni baada ya shirika hilo ambalo lina wajibu wa kusambaza umeme nchini kutangaza rasmi hatua ya kubadilisha jina lake ambapo itakuwa sasa ikiitwa The Kenya Power and Lighting Company Plc.

Umma ulifahamishwa kuhusu mabadiliko hayo mapya kupitia tangazo lililochapishwa na kampuni hiyo kwenye gazeti la Daily Nation, Jumatano, Oktoba 2.

“Notisi imetolewa hapa kuwa shirika la Kenya Power and Lighting Company Limited limebadilisha jina lake ambapo litakuwa The Kenya Power and Lighting Company Plc,”lilisema tangazo hilo.

Aidha, kupitia tangazo hilo, kampuni ilieleza kuwa hatua hiyo iliafikia kufuatia uidhinishaji kutoka kwa Msajili wa Kampuni na maafikiano baina ya wenye hisa.

“…Kufuatia kuidhinishwa inavyostahili na wenye hisa na baada ya kupokea cheti cha kubadili jina kilichotolewa na Msajili wa Kampuni,” ilisema.

Shirika hilo la kusambaza umeme ndilo jipya zaidi kutii Sheria ya 2015 kuhusu Kampuni.

Mnamo Frebruari 2018, kampuni ya mawasiliano ya Safaricom vilevile ilichapisha notisi rasmi kwa umma ikitangaza kubadilisha jina lake kutoka Safaricom Limited hadi Safaricom Public Limited Company (PLC).

Kulingana na sheria hiyo, kampuni ya umma yenye idadi maalum ya hisa zinazohitajika inaweza ikasajilishwa kwa jina linaloishia kwa maneno “kampuni ya umma yenye idadi ndogo ya hisa”.

Kwa upande mwingine, kampuni ambayo ni ya kibinafsi na yenye idadi ndogo ya hisa inaweza kusajilishwa kwa jina linaloishia na “limited” (Ltd)