Habari Mseto

Sababu ya kucheleweshwa kwa mradi wa vipakatalishi

December 5th, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

MAMLAKA ya habari, mawasiliano na teknolojia nchini (ICT), imelaumu kuchipuka kwa shule mpya kila siku kuwa sababu ya kuchelewa mpango wa vipakatalishi.

Afisa Mkuu Mtendaji, Dkt Catherine Gitau alisema mpango huo hauwezi kukamilika kama kila siku kunaanzishwa shule mpya.

Akijibu malalamishi ya walimu wakuu wa shule za msingi wanaokutana mjini Mombasa, Dkt Gitau aliitetea serikali dhidi ya tuhuma za kuchelewesha mradi huo.

“Malalamishi kuwa shule 872 nchini bado hazijapelekewa vipakatalishi miaka sita kupita tangu baadaye, yanatokana na kuwa, kila siku kunaanzishwa shule.

“Sababu nyingine ni kukosekana kwa umeme katika baadhi ya shule hizo,” akasema.Hata hivyo, alisema kuna mipango ua kukamilisha awamu ya kwanza.

Awamu hiyo ilihusisha kusambaza vifaa hivyo katika shule, kutoa mfumo wa mafunzo na kufundisha walimu jinsi ya kutumia vifaa hivyo.

“Katika awamu ya kwanza tumehudumia shule 21,638. Jambo ambalo linarudisha nyuma mradi huu, ni kuzuka kwa shule mpya kila siku. Inatulazimu kuzikagua na kuhakikisha zimesajiliwa kisheria kabla ya kuziingiza katika mradi huu,” akasema.

Awamu ya pili itashughulikia wanafunzi wa darasa la nne hadi la sita.“Wanafunzi watatumia vipakatalishi katika kukuza talanta zao kama mtaala mpya unavyoongoza. Serikali itahakikisha shule ambazo hazitafikiwa na umeme, watatafutiwa mbinu mbadala,” akasema.

Alikanusha madai kuwa kuna baadhi ya walimu ambao bado hawajapata mafuzo ya kutumia vipakatalishi hivyo.