Michezo

Sababu ya mashabiki wa Ingwe kukosa imani na Rupia

February 10th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Mashabiki wa AFC Leopards wamemlia sana mshambuliaji Elvis Rupia baada ya kupoteza penalti timi hiyo ikilimwa na Tusker 1-0 uwanjani Afraha mjini Nakuru kwenye Ligi Kuu, Jumapili.

Rupia, ambaye alijiunga na Leopards almaarufu Ingwe kwa kandarasi ya miezi sita kutoka Wazito FC mwezi uliopita, alikuwa amesifiwa na mashabiki hao alipopachika bao la ushindi katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Ulinzi Stars katika mechi iliyopita.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa zamani wa Nzoia Sugar hakuwa na kismati katika mechi hiyo yake ya pili.

Baada ya Ingwe kupoteza alama zote tatu dhidi ya wanamvinyo wa Tusker, Rupia amelaumiwa. Shabiki Brian Munala alielekeza kidole chake cha lawama kwa mchezaji huyo wa zamani wa Power Dynamos nchini Zambia. “Elvis Rupia anafaa kuondoka timu hii. Nimesikitishwa.” Aliongeza baadaye, “Huwezi kupoteza penalti na utarajie kuibuka na ushindi.”

SirGody E Wes aliuliza kwa kejeli, “Kufunga penalti tu? Yaani kocha hajui nani anafaa kupiga penalti???

“Tulipoteza penalti. Hiki ni kitu kocha anafaa kuangazia kwa makini,” alisema Chris Murunga.

Smith Evans alisema, “Mlipoteza penalti na kisha mnaishia kujutia.”

“Kupoteza penalti kuliua kasi ya AFC Leopards,” alisema Meshack Etindi.

Naye Jonathan Kweyu alirushia Leopards swali, “Mbona mliachilia (John) Makwata? Hii ni aibu.” Penalti ya Rupia ilikuwa ya tatu katika mechi tatu ambayo Ingwe imepoteza baada ya Makwata kupoteza mbili dhidi ya Kisumu All Stars mnamo Januari 25 kabla anunuliwe na miamba wa Zambia, Zesco United.

Baada ya matokeo kati ya Ingwe na Tusker, Tusker imerukia nafasi ya pili kwa alama 41 na kusukuma Kakamega Homeboyz nafasi ya tatu kwa tofauti ya magoli. Mabingwa watetezi Gor Mahia, ambao walizabwa 3-1 na Sofapaka mnamo Februari 8, wanaongoza kwa alama 44. Leopards inapatikana katika nafasi ya sita kwa 34.