Michezo

Sababu ya Mertens kukataa ofa ya Chelsea

June 18th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI mzawa wa Ubelgiji, Dries Mertens alikuwa pua na mdomo na kujiunga na Chelsea mwishoni mwa msimu uliopita.

Licha ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuendelea kumvizia kwa mara nyingine, Mertens amefunguka na kukiri kwamba hana nia ya kuagana na Napoli ambao kwa sasa wamempokeza mkataba mpya wa miaka mitatu.

“Karibu nishawishike kutua uwanjani Stamford Bridge muhula jana kuvalia jezi za Chelsea waliojaribu kunishawishi kwa ofa nono za kila sampuli,” akatanguliza Mertens.

“Lakini unapopata makazi ya kudumu katika eneo lolote la Kusini mwa Italia, uchukuliwe kama mungu na wengi wa mashabiki wako na upate kiasi fulani cha fedha zinazokuridhisha; mbona utake zaidi?” akauliza mshambuliaji huyo.

“Ningeyoyomea Chelsea kisha ‘nisiwe mtu yeyote’ katika EPL. Mbona nijitakie makuu ilhali nyota yangu yaendelea kung’aa zaidi kambini mwa Napoli nchini Italia?” akaongeza.

Mertens, 33, aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Napoli mnamo Juni 13 baada ya bao lake dhidi ya Inter Milan ya kocha Antonio Conte kuwakatia waajiri wake tiketi ya fainali ya Coppa Italia msimu huu.

Kufikia sasa, anajivunia jumla ya mabao 122, moja zaidi kuliko Marek Hamsik wa Slovakia aliyekuwa akitoshana naye hadi Napoli waliposhuka dimbani kuvaana na Inter.

Mertens alihiari kurefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa Napoli licha ya kuhemewa pakubwa na Chelsea na Inter ambao walipania sana kumfanya kizibo cha Lautaro Martinez anayepigiwa upatu kutua Uhispania kuvalia jezi za Barcelona muhula ujao.

Kubwa zaidi ambalo awali lilitarajiwa kumshawishi Mertens kubanduka Napoli na kutua Uingereza ni ukubwa wa mapenzi yake kwa jiji la London ambako amekuwa na mazoea ya kuzuru mara kwa mara na mkewe kila anapokuwa likizoni.

Hilo liliwafanya Chelsea kuanza kumwandama usiku wa mchana licha ya kujivunia tayari maarifa ya sajili wapya Hakim Ziyech na Timo Werner watakaoshirikiana na Olivier Giroud na Tammy Abraham katika safu ya uvamizi msimu ujao. Ziyech na Werner walisajiliwa kutoka Ajax (Uholanzi) na RB Leipzig mtawalia.