Kimataifa

Sababu ya serikali kukataa kusajili gari la Dave Assman

February 11th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME kutoka Canada ambaye jina lake linatoa taswira ya lugha chafu anapambana aruhusiwe kusajili gari lake, baada ya serikali kukataa kusajili gari hilo kutokana na jina lake la mwisho ‘Assman’.

Bw Dave Assman, wa miaka 47, amekuwa akijivunia jina lake hilo na kusema anavyolipenda, japo sasa haelewi sababu ya serikali kukataa kusajili gari lake kwa jina hilo.

Mwanamume huyo alikuwa akitaka kuwekewa jina hilo katika nambari ya kutambulisha gari (number plate).

“Nilipigia afisi hiyo na nikawaambia sio matamshi, ni jina langu. Walisema wameelewa lakini watu wengine hawataelewa na hivyo watahisi ni ukosefu wa maadili,” akasema Bw Assman.

Kulingana na sera za idara ya kusajili magari nchini humo, nambari ya kibinafsi haiwezi kusajiliwa ikiwa jina linalotumiwa ni la matusi ama ambalo linaweza kutafsiriwa vibaya.

Msemaji wa idara hiyo Tyler McMurchy alisema kuwa sheria hiyo inafanya kazi hata ikiwa jina hilo ni la mtu na linatamkwa kwa namna nyingine tofauti na lilivyoandikwa. Hii ilikuwa baada ya mwanamume huyo kudai kuwa huwa anajiita Bw ‘Ossman’.

Bw Assman alianza kujaribu kupewa usajili huo miaka 20 iliyopita, ambapo alikatazwa kutokana na jina lake.

“Nilijaribu tena majuzi na nikjaambiwa haikubaliki kwani ni matamshi ya kuchukiza. Nilitaka kujua ikiwa nafaa kubadili jina,” akaendelea kusema.

Alisema kuwa analiheshimu jina hilo sana kwani linamuunganisha na babu yake wa kale ambaye alikuwa mkulima hodari katika mkoa wa kwao.

Lakini jina Assman si geni haswa nchini Marekani, kwani mnamo 1995, mtangazaji wa runinga David Litterman alifanya mahojiano na mwanamume aliyeitwa Dick Assman, mtu wa familia ya Assman wa sasa.