Habari

Sababu ya serikali kuweka mpango wa kuwapa wanafunzi kondomu

February 18th, 2019 2 min read

Na CHARLES LWANGA

SERIKALI itawapa wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo mipira ya kondomu katika juhudi za kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi miongoni mwa vijana.

Kulingana na Naibu Mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Kupambana na Ukimwi (NACC), Bw John Kimigwi, hatua hii imechukuliwa baada ya kufahamika kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 ndio wanaothiriwa zaidi na maambukizi ya Ukimwi.

Wengi wa walio katika umri huu ni wanafunzi wa sekondari na vyuo.

Wakati mpango sawa na huu ulipotangazwa mnamo 2014, walimu waliushtumu vikali wakisema hatua hiyo ingewafanya wanafunzi kushiriki ngono kiholela. Maoni sawa na hayo yalitolewa na kanisa Katoliki pamoja na wazazi.

Ripoti kuhusu maambukizi ya Ukimwi inaonyesha kuwa kati ya vifo 52,000 vilivyotokana na Ukimwi mnamo 2017, vijana wa umri huu walikuwa 17,000. Hiyo ni zaidi ya robo ya watu wote waliaga dunia kutokana na maradhi hayo.

Akizungumza katika sherehe ya kuadhimisha siku ya kondomu ulimwenguni nje ya Chuo Kikuu cha Pwani mjini Kilifi, Bw Kimigwi alisema vijana wa kati ya miaka 15 na 24 wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi licha ya ripoti kuonyesha kuwa ukimwi umepungua nchini kwa asilimia 40.

Bw Kimigwi alisema kuwa mipira hiyo pia itachangia katika kupunguza mimba za mapema akieleza kuwa mimba za mapema katika Kaunti ya Kilifi zimeongezeka kutoka 13,000 hadi 17,850 katika kipindi cha miezi mitano pekee.

“Hii inaonyesha jinsi uambukizaji wa virusi vya Ukimwi unavyoongezeka kwa sababu hakuna matumizi ya mipira ya kondomu hapa Kilifi, ambayo pia imeorodheshwa kuwa kati ya kaunti maskini nchini,” alisema.

Bw Kimigwi alieleza matumaini kuwa kwa kuwapa vijana wa shule za sekondari na vyuo mipira ya kondomu pamoja na kampeni ya matumizi yake, maambukizi ya HIV nchini yatapungua.

“Tunafaa tuungane kulinda vijana walio chini ya miaka 24 ili tupate kizazi chenye afya siku za usoni,” alisema.

Alisema tayari wameanza kufanya kampeni ya matumizi ya kondomu kupitia kwa mitandao ya kijamii na vijana wenyewe ili waelimishe wenzao.

Kwa upande wake, Bi Maureen Mwangovya, ambaye ni waziri wa jinsi katika Kaunti ya Kilifi alisema uambukizaji wa virusi vya Ukimwi katika kaunti hiyo ni asilimia 38 huku wengi wa waathiriwa wakiwa ni wasichana.

“Ni vyema kuchukua hatua ya kupunguza mimba za mapema kwa sababu vijana wa kati ya umri ya miaka 15 hadi 19 wamekuwa wakiambukizana virusi vya Ukimwi kwa sababu hawatumii kondomu,” alisema.

Bi Mwangovya pia alisema wametambua sehemu kama mikahawa na mahali pa vileo ambapo wanapanga kuweka mipira za kondomu ili kupunguza maambukizi ya HIV.

Wakati wa maadhimisho hayo, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Pwani, waendeshaji bodaboda na makondakta wa matatu waligawiwa mipira ya kondomu.