HabariSiasa

Sababu ya Uhuru kumfuata Ruto kanisani

December 9th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

Wakenya wengine walishangaa kwa nini mchango wake ulitangazwa, ilhali Kanisa Katoliki lilitoa masharti mapya kuhusu harambee kwamba michango inafaa iwe siri ili isitumiwe na viongozi kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

RAIS Uhuru Kenyatta ameanza kufuata nyayo za naibu wake William Ruto katika juhudi za kujenga umaarufu wake uliodidimia eneo la Mlima Kenya.

Katika juhudi hizi, Rais Kenyatta ameanza kumuiga Dkt Ruto kwa kuhudhuria hafla makanisani na kuchangisha pesa.

Hapo Jumapili alihudhuria misa katika Kanisa Katoliki la St Francis of Asisi mjini Ruiru, Kaunti ya Kiambu kisha akashiriki harambee ya ujenzi wa kanisa jipya na akatoa mchango wa Sh3 milioni, na kuahidi kuongeza Sh4 milioni baadaye, kwa mujibu wa kitengo cha habari cha Ikulu (PSCU).

Hii ilikuwa mara ya pili katika muda wa wiki moja kwa Rais kuhudhuria hafla ya kimaendeleo eneo la Kati baada ya kipindi kirefu cha malalamishi ya viongozi na wakazi wa Mlima Kenya kwamba amewapuuza.

Mbinu hiyo ya kushiriki hafla za makanisa imekuwa ikiendelezwa zaidi na Dkt Ruto hasa katika eneo la Kati ambako hafla zake nyingi zimeongeza umaarufu wake kwa wakazi.

Kwa upande mwingine imekuwa nadra sana kwa Rais Kenyatta kushiriki katika harambee kwa muda mrefu sasa, na washirika wake wamekuwa wakimlaumu Dkt Ruto na hata kushutumu michango anayotoa.

Badala ya kushiriki harambee moja kwa moja, wakati mwingine Rais Kenyatta amekuwa akiwaita wasimamizi wa shule na wanafunzi katika Ikulu ya Nairobi ambapo huwa anawakabidhi mabasi ya shule yanayogharimu mamilioni ya pesa.

Hatua yake ya Jumapili kushiriki harambee kanisani ilifanya wengi kujiuliza imekuwaje akafuata mkondo wa Dkt Ruto ambao wandani wake wamekuwa wakishutumu.

“Wale waliokuwa wakimkashifu Naibu Rais kwa kufanya harambee kanisani, mko wapi?” akauliza mtumizi wa mtandao wa Twitter aliyejitambulisha kama @evans_ndaiga.

Naye @BryanSangRutto akasema: “Hatimaye Uhuru amekubali harambee si jambo baya.”

Wakenya wengine walishangaa kwa nini mchango wake ulitangazwa, ilhali Kanisa Katoliki lilitoa masharti mapya kuhusu harambee kwamba michango inafaa iwe siri ili isitumiwe na viongozi kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Katika hotuba yake, Rais Kenyatta alitilia mkazo hitaji la Wakenya kuungana katika vita dhidi ya ufisadi ambao alisema ni kikwazo kikuu kwa maendeleo ya nchi.

“Tafadhali tusiingize siasa katika vita dhidi ya ufisadi. Wakati mtu akipora mali ya umma huwa hafanyi hivyo kwa niaba ya familia yake wala jamii. Kwa hivyo mtu yeyote anayeshtakiwa anafaa kubeba msalaba wake mwenyewe,” akasema.

Aliongeza kuwa kisheria asasi zote zinazohusika katika kupambana na ufisadi hazifai kuingiliwa na yeyote na kwamba, kila anayeshtakiwa anapaswa kuchukuliwa kuwa asiye na hatia hadi wakati mahakama itakapoamua kwamba ana hatia.

“Kama taifa linalotii sheria, inafaa turuhusu asasi zetu zilizotwikwa jukumu la kupambana na ufisadi zifanye kazi zao kwa uhuru na kuhakikisha hakuna ubaguzi kwa washukiwa,” akasema.

Matamshi hayo yalitokea huku Gavana wa Nairobi, Mike Sonko akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Rais alikuwa ameandamana na viongozi wengine wakiwemo Naibu Gavana wa Kiambu James Nyoro, ambaye anashikilia usimamizi wa kaunti hiyo kufuatia uamuzi wa mahakama kwamba Gavana Ferdinand Waititu hastahili kuingia afisini hadi kesi yake ya ufisadi itakapokamilika.

Rais pia alitoa wito kwa wananchi kuwa na umoja kuanzia katika familia zao ili kukuza maadili ya kitaifa.