Makala

Sababu ya vishoroba vya Lamu kusalia mahame mchana

May 4th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

MISONGAMANO ya watu, punda na mikokoteni ni jambo la kawaida kushuhudiwa kwenye Mji wa Kale wa Lamu.

Hali hiyo mara nyingi hushuhudiwa sana asubuhi na mapema au nyakazi za jioni.

Hili linatokana na kigezo kwamba miundomsingi, hasa barabara za waja, punda na mikokoteni kupitia kwenye mji huo wa kihistoria ni za vichochoro au vishoroba tu.

Ni kwenye Mji wa Kale wa Lamu ambapo magari, baiskeli, pikipiki na mifumo mingine ya uchukuzi wa kisasa hairuhusiwi.

Ni marufuku inayowapasa wanakisiwa kutoikaidi kamwe katika kile kinachozingatiwa kuwa ni kuhifadhi hadhi ya mji huo wa kale, ambayo mambo yake ni ya kizamanizamani.

Ikumbukwe kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), mnamo 2001 liliuorodhesha Mji wa Kale wa Lamu kuwa miongoni mwa maeneo yanayotambuliwa zaidi ulimwenguni kwa kuhifadhi mila, tamaduni na ukale wake-yaani Unesco World Heritage Site.

Licha ya suala la misongamano ya kila mara kushuhudiwa kwenye Mji huo wa Kale, jambo ambalo huenda likakuacha na mshangao ni endapo utapata mwanya wa kuzurura kwenye vishoroba vya katikati ya mji huo nyakati za mchana, hasa majira ya adhuhuri yanapowadia.

Hapa, mja huenda akadhania anatembea kwenye eneo lililo mahame kwani vishoroba vingi vya mji huo wa kale husalia pweke.

Kelele na zahama ambazo hushuhudiwa asubuhi na jioni hukosekana kabisa nyakati hizi.

Mandhari ya vishoroba hivyo vya Mji wa Kale wa Lamu mchana hugeuka na kuwa tulivu kiasi cha kusikia michakato ya nyayo zako unapotembea.

Je, wakazi waliozoeleka kuzururazurura kwenye vinjia hivyo huwa wameenda wapi? Ni sababu ipi hasa inayopelekea vishoroba vya Lamu kusalia mahame mchana?

Katika mahojiano na Taifa Leo, wanakisiwa walisema ni mazoea yao kuamka asubuhi na mapema ili wa kuenda sokoni aende na wa kazini naye awahi kufika ofisini kwake wakati ufaao.

Kimojawapo cha vishoroba vya mji wa Lamu kikiwa na msogamano wa watu na punda. Misongamano mara nyingi hushuhudiwa asubuhi na jioni ilhali mchana kukishuhudiwa upweke vishorobani. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Abdulrahman Salim anasema kutokana na hali ya vishoroba ilivyo mjini, wanaokwenda kazini na sokoni huishia kukutana kwenye vishoroba hivyo vyembamba, hivyo kuchangia misongamano ishuhudiwayo.

“Kinyume na miji mingine ya Kenya, Lamu ni mji wa kale ambao vijia vyake ni vyembamba. Asubuhi wengi huchangamkia shughuli za siku. Wale wanaoenda kazini au sokoni huishia kukutanika kwenye vibaraste vyetu, hivyo kuishia kusongamana,” akasema Bw Salim.

Aliendelea kwa kueleza kuwa jioni pia lazima hali hiyo ya misongamano iwepo kwani wengi ambao huwa wamevuka upande mwingine wa Lamu kama vile Mokowe kufanya kazi huanza kurudi makwao.

“Wengi wa wanaoishi Lamu hufanya kazi Mokowe, Mpeketoni na sehemu nyingine zilizoko nje ya kisiwa. Hilo linamaanisha jioni wanaporudi mjini huongeza idadi ya watumiaji wa vishoroba vyetu, hivyo kuishia misongamano kushuhudiwa,” akasema Bw Salim.

Naye Bi Maryam Mzee, anasema mbali na watu wengi kuvuka maeneo ya nchi kavu, nje kabisa ya kisiwa cha Lamu kufanya kazi mchana, sababu nyingine kuu inayofanya vichochoro vya Mji wa Kale wa Lamu kukosa watu ni kwamba wengi huwa wamebarizi kwa nyumba zao au misikitini wakitekeleza swala na ibada.

Ikumbukwe kuwa Mji wa Kale wa Lamu ni ngome ya dini ya Kiislamu.

Idadi kubwa ya wanaoishi mjini humo ni jamii ya Waswahili wa asili ya Wabajuni.

Bi Mzee anasema badala ya waja kurandaranda kiholela mitaani, wengi huishia kuswali misikitini na kisha kuingia kwa nyumba zao kupumzika au kula.

“Tabia ya watu wetu Wabajuni hapa ni kwamba mchana hupumzika, walale, iwe ni majumbani mwao au misikitini. Huwezi kumpata mja akitembea ovyo jua likiwaka hapa. Na ndio sababu ukaona mitaa yetu ikikaa kama mahame mchana,” akasema Bi Mzee.

Bw Benson Kamau amabye ni hamali mjini Lamu anasema matajiri wao wengi ni Waislamu na kwamba ifikapo adhuhuri, wao pia hulazimika kupaki mikokoteni yao wakiwasubiri mabosi wao wamalize kuswali misikitini na kupumzika mchana kabla ya kuendelea na kazi majira ya alasiri.

“Pengine kuna wale ambao watajiuliza hii mikokoteni au punda huwa wako wapi mchana. Sisi mahamali pia huishia kupumzika adhuhuri. Waajiri wetu huwa misikitini wakiswali na hutupa breki kwanza hadi wamalize maombi yao. Ndo pia ukapata hutuoni njiani na mikokoteni mchana,” akasema Bw Kamau.

Mji wa Kale wa Lamu ni miongoni mwa sehemu zinazounda kisiwa cha Lamu.

Maeneo mengine ni Shela, Kashmir, Hidabo, Kandahar, Bombay, India, Makafuni, Matondoni na Kipungani.

Kisiwa cha Lamu kwa jumla ni makazi ya zaidi ya watu 30,000.