Makala

Sababu ya wengi katika sekta ya kilimo kuomba bei ya petroli izidi kupanda

March 1st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

BEI hasi ya bidhaa za petroli imezua mwamko mpya wa ubunifu katika kilimo cha unyunyiziaji mimea maji ambapo wakulima sasa wanatumia gesi kama nishati mbadala.

Bei ya mafuta ya petroli na dizeli ambayo sanasana hutumika katika upigaji maji kutoka viini vyake hadi kwa mashamba ilianza kupanda baada ya serikali kupandisha ushuru wa inaotoza bidhaa hizo katika mswada wake wa Kifedha wa 2023.

Bw Bernard Muthike ambaye ni mkulima katika kijiji cha Gatitika kilichoko Kaunti ya Kirinyaga anasema kwamba gesi ya kilo sita ambayo gharama yake ni kati ya Sh1,000 na Sh1,200 humfaa kunyunyizia mimea ambayo petroli ya Sh4,000 ingetumika.

“Ni vyema waliongeza bei ya petroli kwa kuwa singegundua mwanya huu wa faida. Ina maana kwamba ninaokoa zaidi ya Sh2,800 kwa mpigo mmoja. Kwa sasa sina haja ya kujua bei ya petroli imefika wapi,” akasema.

Anasema hushirikisha kilimo cha unyunyiziaji katika ekari mbili na ndizo hutumia Sh1,200 kama gharama ya wiki moja.

Bw Bernard Muthike (kushoto) akiwa na mwenzake Bw Dennis Kariuki. PICHA | MWANGI MUIRURI

Bw Dennis Kariuki ambaye ni kibarua katika eneo hilo anasema kwamba ubunifu wa kuunganisha mtungi wa gesi na jenereta ni wa kusisimua na ilibidi kwanza waite wataalamu wa kuwaonyesha jinsi hufanyika.

“Ubunifu huu ulianza kama fununu tu wakati mjadala wa Rais William Ruto kuhusu pikipiki na magari ya kutumia stima badala ya petroli ulizuka. Ndipo baadhi ya wenyeji walio na ufahamu wa nguvu za nishati walianza kutuhamasisha kwamba hata gesi inaweza ikatumika katika kilimo,” asema Bw Muthike.

Bw Muthike anaongeza kwamba wakulima walioanza kukumbatia ubunifu huo walizidisha kuupigia debe wakisema jinsi walivyokuwa wakiokoa pesa na kila mkulima akaanza kukimbizana na utaalamu huo.

Wauzaji mitungi ya gesi katika miji ya mashinani wameripoti biashara ya faida kutokana na ubunifu huo.

“Kwa mwezi sasa ninauza zaidi ya mitungi 100 kutoka kiwango cha awali cha mitungi 20 pekee. Natoa huduma za kujaza mitungi hiyo gesi kwa kiwango cha idadi ya 200 kutoka chini ya mitungi 100 miezi sita iliyopita. Ubunifu huu umenifaa kibiashara,” asema Bw James Kiragu ambaye hufanya biashara yake katika mji wa Ngurubani.

Kwa upande wake, fundi wa mitambo ya jenerata Bw John Muiruri anasema kwamba amekuwa na kazi ya kufana akitembea mashinani akisaidia wakulima kuunganisha mitambo ndio washirikishe unyunyiziaji.

“Sio kazi ngumu na imeniinua si haba. Mkulima akiwa na jenereta na mtungi wa gesi anahitajika tu kununua vifaa vya gharama ya Sh1,200 ndio ahamie katika teknolojia hii mpya. Mimi nitatoza zangu Sh2,000 ambazo zinajumuisha kukupa elimu ya jinsi ya kutumia mitambo hiyo kwa njia salama na pia uhamasisho wa kiufundi iwapo utapata hitilafu isiyo kubwa,” asema.

Bw Muiruri anasema kwamba kati ya Septemba 2022 na Februari 2024 alikuwa amehudumia wakulima 347 katika Kaunti za Murang’a, Kirinyaga, Embu, na Nyeri.

Anasema kwamba hangetaka bei ya petroli ishuke “kwa kuwa kufanya hivyo ni kunifukarisha pamoja na wengine wengi ambao wamejipata katika riziki ya faida”.

[email protected]