Habari Mseto

Sababu ya Zuleikha Hassan kuingia bungeni na mtoto

August 9th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

MWAKILISHI wa Wanawake wa Kaunti ya Kwale katika Bunge la Kitaifa, Bi Zuleikha Hassan amefichua kwamba alikiuka kimakusudi sheria zinazopiga marufuku wageni kuingia katika ukumbi wa mijadala alipofurushwa baada ya kuiingia na mtoto wake mwenye umri wa miezi mitano.

Mbunge huyo ambaye ni mama wa watoto watatu alisema kwamba alifanya hivyo baada ya kuchoshwa na hali ya taasisi hiyo kutokuwa na mazingira yanayofaa kwa kina mama wachanga.

“Huyu akiwa mtoto wangu wa tatu ambaye nimepata nikiwa bungeni, nilichoshwa tu na hali ya taasisi hiyo kutokuwa na mazingira yanayowafaa kina mama wachanga. Nilijua hairuhusiswi lakini nilihisi tu kuchoshwa na hali hiyo,” alisema Bi Hassan.

Akizungumza na vyombo vya habari katika chumba maalum cha watoto kilichotengewa wahudumu wa kike bungeni, na ambacho kilifunguliwa kwa mara ya kwanza kwa wanahabari mnamo Alhamisi, Bi Hassan alikanusha madai ya kuwepo chumba hicho maalumu kilichobuniwa 2013 na Tume ya Huduma za Bunge (PSC), akisema zilikuwa njama za baadhi ya viongozi kumuaibisha.

“Baadhi ya viongozi bungeni pengine wanajaribu kunifedhehesha kwa kusema kumekuwepo na chumba hicho mbeleni. Kwa nini sikujua hivyo hapo mbeleni na nimekuwa nikipata watoto na huwa wanafahamu. Hakuna mbunge mwingine anayefahamu kuhusu chumba hicho wala mfanyakazi wa bunge ambaye amewahi kupata mtoto anayejua kuhusu chumba hicho,” alifunguka.

Bi Hassan aligonga vichwa vya habari nchini na vya kimataifa alipoandikisha historia kwa kufurushwa bungeni baada ya kuingia akiwa amebeba mtoto wake mchanga kinyume na sheria za bunge zinazozuia watu wasiojulikana kuingia majengo ya bunge katika kisa kilichoibua hisia kali nchini na kimataifa.

Kitendo chake kilifanya usimamizi wa bunge kuchukua hatua ya dharura na kuandaa chumba hicho cha watoto kilicho umbali wa kilomita 400 kutoka majengo ya bunge na ambacho hakijawahi kutumika tangu kilipoanzishwa.

“Nina furaha kwamba bunge lilichukua hatua ya haraka sana kwa sababu tunaweza kuona vitu vingi ni vipya na kwa kweli kinanuka upya. Hata hakijatumika nashuku hakuna mtu ambaye amewahi kukitumia.

Hata hivyo alilalamika kuhusu umbali wa chumba hicho akisema haukufaa kwa wabunge wanawake ambao watalazimika kwenda mwendo mrefu kuwanyonyesha watoto wao ilhali kulikuwa na kilabu kilichojengwa kando ya bunge.

“Tatizo tu ni kwamba chumba hiki kiko mbali sana. Kama sasa kuna baa iliyo kando na bunge. Lakini sisi wenye watoto tutalazimika kutembea kwa mwendo mrefu ili kumnyonyesha mtoto kila mara msaidizi wako anapokuambia mtoto analia. Mwendo huo wa kwenda na kurudi utatufanya kukosa sehemu kubwa ya vikao vya bunge,” alisema.

Kufuatia kitendo, hicho, Bi Hassan alitakiwa kujiwasilisha mbele ya Kamati kuhusu Mamlaka na Kibali cha Bunge inayooongozwa na Spika Justin Muturi kuelezea ni kwa nini alienda kinyume na sheria za bunge.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema yuko tayari kuikabili kamati hiyo kwa sababu alikuwa akipigania haki za kina mama wachanga bungeni hivyo basi alikuwa tayari kwa matokeo.

Kitendo cha kumrusha nje ya bunge Bi Hassan na mtoto wake wa miezi mitano kiliibua ghadhabu nchini na katika nyanja za kimataifa huku Rais wa Shirika la Sheria Kenya (LSK) Bw Allen Gichuhi akiitaka serikali kuwaomba radhi Wakenya na kubuni sera zitakazohakikisha utekelezaji wa Sheria kuhusu Unyonyeshaji pamoja na Kuwalinda kina mama wanaonyonyesha katika sehemu za kazini.