Afya na Jamii

Sababu za akina mama wajawazito kuogopa kliniki za uzazi

May 19th, 2024 4 min read

NA JESSE CHENGE

WASIWASI unaongezeka Kaunti ya Bungoma kufuatia imani ya jadi ya Bukusu kwamba wanawake wajawazito wanapaswa kufungiwa majumbani mwao.

Hili linaweka presha kwa wajawazito ambao mwishowe huogopa kuhudhuria kliniki za uzazi (ANC) kufuatilia afya ya mama na mtoto tumboni.

Hali hii inaathiri vibaya ushiriki wao katika kliniki za uzazi licha ya wao kukabiliwa na hatari ya kukosa chanjo muhimu na mawaidha megine kuhusu kulea mimba na lishe bora.

Bungoma ni miongoni mwa kaunti zenye maambukizi ya juu ya malaria, hali inayoleta hatari kubwa kwa wanawake wajawazito, wazee, na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Bi Jentrix Kima, 36, ambaye ni mama wa watoto watatu kutoka kijiji cha Lukhuna katika eneobunge la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma, ni mmojawapo wa wanawake ambao maeneo wanakotoka, ni kama ni mwiko mwanamke mtu mzima kuhudhuria kliniki hizo za ANC.

Anadai kwamba umuhimu wa vituo vya afya kwa wajawazito haupewi kipaumbele, na aliwahi kuonywa dhidi ya kwenda kliniki wakati wa ujauzito wake.

Kwa Bi Kima, kupambana na malaria na kutafuta matibabu katika kituo cha afya ilikuwa changamoto kubwa kutokana na baadhi ya mila kandamizi.

Baadhi ya hizo mila kandamizi anasema ni kwamba kwenda kliniki za ANC kulionekana ni kudunisha utu wa mwanamke ikitokea kwamba angehudumiwa na muuguzi ambaye ni mwanagenzi wa taasisi ya mafunzo ya matibabu.

Pia anaeleza kwamba katika dunia ya kisasa, baadhi ya wanawake, waliogopa kwamba wasichana wanaopachikwa mimba wakiwa matineja ni wengi, hivyo kuna uwezekano wa mama na binti yake kuhudhuria kliniki moja, jambo ambalo baadhi ya wanajamii wanashikilia ni la aibu.

Aidha, changamoto nyingine ni kwamba mwanamke mjamzito hudhaniwa akienda hospitalini na kuzoeana na madaktari na wahudumu, huenda akashawishika kuwekewa namna ya kupanga uzazi hata bila kuhusisha mume wake.

Bi Jentrix Kima wa kutoka katika kijiji cha Lukhuna. PICHA | JESSE CHENGE

Bi Kima anasema yeye mwenyewe amewahi kujipata njia panda kwa sababu ya presha za aina hiyo, lakini baada ya kupokea taarifa na maelezo kutoka kwa mvumishaji wa afya ya jamii (CHP) kuhusu umuhimu wa vipimo vya malaria na ziara za ANC, aliamua kutafuta msaada katika kituo kimojawapo cha afya.

“Baadhi yetu kabla ya kuwaelimisha wanafamilia kuelewa unuhimu wa kufanyiwa vipimo na kupewa dawa za virutubishi, tulikuwa tunaambiwa tulee tu mimba huku tukichunga mifugo nyumbani,” asema Bi Kima.

Anaongeza kwamba ilijengeka imani potofu kwamba kujiandaa kwa kuzaliwa kwa mtoto hakuhitajiki na kunaweza hata kuleta mkosi au kusababisha kifo cha kimalaika tumboni.

“Mama mkwe wangu na mume wangu, awali waliogopa jaribio la kununua taulo na nguo kwa ajili ya mtoto niliyemtarajia, wakiogopa matokeo mabaya,” aeleza.

Akiwa na ujauzito wa miezi sita, Bi Kima alitembelewa na CHP ambaye alimshawishi kuanza kuhudhuria kliniki kwa vipimo vya malaria na ziara za ANC. Katika kituo cha afya, alipokea matibabu sahihi na alipewa neti iliyotibiwa ili kumlinda yeye na mtoto wake tumboni dhidi ya kuumwa na mbu na kuambukizwa malaria. Mume wake alimfuata wakati wa ziara muhimu hii.

Licha ya uzoefu wake mzuri, Bi Kima alifichua kwamba hakuwa amehudhuria kliniki za ANC wakati wa ujauzito wake wa kwanza na wa pili kutokana na dhana potofu kama hizo zilizosambazwa na wanajamii.

Mama huyo sasa anawahimiza wanawake wajawazito kutembelea vituo vya afya kwa huduma maalum, kwani alipokea taarifa muhimu kuhusu uzazi wa mpango na huduma ya mtoto mchanga wakati wa ziara zake za ANC ambazo alikosa wakati wa ujauzito wake wa kwanza na wa pili.

“Kuna taarifa muhimu kuhusu uzazi wa mpango na huduma ya mtoto mchanga ambazo wanawake wajawazito wanaweza kupokea tu kwa kuhudhuria kliniki. Ni muhimu kuhudhuria kliniki zote hadi kufikia siku ya kujifungua,” aongeza.

Anajuta kwamba wakati wa ujauzito wake wa kwanza na wa pili, alikuwa mara kwa mara anaugua, hivyo kuweka hatari kwa yeye na watoto aliotarajia wakati huo.

Katika kijiji cha Lukhuna, Bi Kima anathibitisha kwamba wanawake wajawazito bado wanahofia kutembelea vituo vya afya kwa matibabu ya malaria na ziara za ANC.

Kwa lengo la kukabiliana na dhana potofu kama hizi katika jamii za Bungoma, shirika la Breakthrough Action limechukua jukumu la kuelimisha jamii na watoa huduma za afya, lengo likiwa ni kusambaratisha uongo huu na kuwahimiza wajawazito kuenda zahanatini kufanyiwa vipimo vya malaria na vilevile kufanya ziara za ANC.

Afisa wa Mabadiliko ya Tabia za Jamii na Uhusishaji wa Jamii katika shirika la Breakthrough Action Bw Isaac Juma anasema imani potofu kuhusu matumizi ya neti za kuzuia mbu na msimamo hasi kuhusu ziara za ANC ni kawaida Bungoma.

Bw Juma anasema azma ya shirika hilo ni kupiga jeki wanajamii na vituo vya afya kukabili dhana potofu hizi kupitia ushirikiano.

Bw Juma alisema kwamba baadhi ya wanawake wajawazito huwa na hofu kutembelea kliniki kutokana na kutaka kuhifadhi ujauzito wao kwa siri.

Afisa wa Breakthrough Action Bw Isaac Juma. PICHA | JESSE CHENGE

Pia alibainisha kwamba baadhi ya wanawake hujitokeza ANC wakati mimba ni ya miezi saba, ambayo inachukuliwa kuwa ni kuchelewa sana.

Breakthrough Action inashirikiana na washirika wengine wa kupambana na malaria, kama vile Afya Ugavi na KANCO, kusaidia mikakati mbalimbali katika mapambano dhidi ya malaria, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa dawa, bidhaa za kupambana na malaria, na kufuatilia kaya mbalimbali kwa ukaribu.

Bw Moses Wambusi, ambaye ni mratibu wa masuala kuhusu malaria katika Kaunti, anaripoti kiwango cha kuenea kwa asilimia 29.

Viwango vya kuenea kwa malaria kwa mwaka 2023 na 2024 ni kama ifuatavyo Bumula (asilimia 49), Cheptais (asilimia 27), Kabuchai (asilimia 34), Kanduyi (asilimia 20), Kimilili (asilimia 19), Mt Elgon (asilimia 8), Sirisia (asilimia 46), Tongaren (asilimia 12), Webuye Mashariki (asilimia 25), na Webuye Magharibi (asilimia 28).

Nchini Kenya, kuna makadirio ya visa 3.4 milioni na vifo 11,800 kila mwaka, na wale wanaoishi magharibi mwa Kenya wana hatari kubwa ya kupata malaria.

Kama ilivyo katika nchi nyingi ulimwenguni, Kituo cha Kukabiliana na Kusambaa kwa Maradhi cha Amerika (CDC) kimefanya kazi kwa karibu na Wizara ya Afya ya Kenya kupambana na malaria.

Zaidi ya miaka minne iliyopita, CDC iliweka ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kuhusu Matibabu nchini Kenya (Kemri).

Karibu kila dakika, mtoto chini ya umri wa miaka mitano anakufa kutokana na malaria.

Vifo vingi kati ya hivyo vinaweza kuzuilika na kutibika.

Mwaka 2022, kulikuwa na jumla ya visa 249 milioni za malaria ulimwenguni ambavyo vilisababisha vifo 608,000 kwa ujumla. Kati ya vifo hivyo, asilimia 76 vilikuwa vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Hii inamaanisha kufikia idadi ya watoto zaidi ya 1,000 chini ya umri wa miaka mitano kila siku.

Wengi wao, wanaoishi kusini mwa jangwa la Sahara, wako katika hatari ya kupata malaria na kukabiliana na changamoto zake za kiuchumi.

Licha ya mzigo mkubwa wa malaria katika afya na uchumi, maendeleo makubwa yalifanyika dhidi ya ugonjwa huo kuanzia mwaka 2000 hadi 2019 kutokana na ongezeko la fedha na programu za kukabiliana na ugonjwa huo. Kati ya mwaka 2000 na 2019, viwango vya vifo vinavyotokana na malaria vilipungua kwa nusu kutoka 28.8 hadi 14.1 kwa kila watu 100,000 wenye hatari ya kuathiriwa.

Mwaka 2020, kiasi cha vifo kiliongezeka hadi 15.2 kwa kila watu 100,000 wenye hatari hii.