Habari Mseto

SHAMBULIO: Sababu za Al Shabaab kulenga hoteli ya Dusit D2

January 17th, 2019 2 min read

Na WYCLIFFE MUIA

HOTELI ya Dusit D2 ndio ilikuwa kitovu cha shambulizi la kigaidi Jumanne na wengi wameanza kuhoji sababu za magaidi kulenga hoteli hiyo iliyoko kwenye mtaa wa hadhi ya juu wa Lavinghton, Nairobi.

Dusit D2 ambayo ina makao yake makuu jijini Bangkok, ilifungua tawi lake jijini Nairobi mnamo 2014 katika barabara ya Riverside 14.

Hoteli hiyo inayomilikiwa na familia ya Sanghrajka inayomiliki pia biashara za Tile & Carpet Centre, ilishinda tuzo la ‘The Best Luxury Business Hotel’ 2018 katika kanda ya Afrika Mashiriki.

Wachanganuzi wasema huenda magaidi walilenga hoteli hiyo kwa sababu ya kuandaa kongamano na shughuli nyingi zinazohusisha wageni wengi wa kimataifa.

“Magaidi wanapenda mahali kuna wageni wengi wa kigeni ili maovu yao yawezwe kumulikwa kimataifa. Hata mjini Mogadishu, hoteli nyingi zinazoshambuliwa ni zile zenye raia wa kigeni na afisi za Umoja wa Mataifa,”anasema mtaalamu wa maswala ya usalama, Simiyu Werunga.

Kulingana na Bw Werunga, ilikuwa rahisi kwa magaidi kupanga shambulio hilo kutokana na shughuli nyingi za wageni zinazoendelea katika hoteli hiyo.

Barabara ya Riverside Drive, ina shughuli nyingi kutokana na kuwepo kwa afisi kadhaa za mabalozi mbalimbali na benki kadhaa. Vilevile, eneo hilo pia linatembelewa na idadi kubwa ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi bewa la Chiromo.

Hata hivyo, mtaalamu mwingine wa masuala ya usalama Antony Njeru anahisi DusitD2 ilijianika sana kwa kuchapisha habari muhimu za kiusalama katika tovuti yake.

“Inaonekana magaidi walipata ramani yote ya Dusit Complex katika tovuti yao. Ni makosa kutoa maelezo ya kina kuhusu maeneo ya kiusalama ndani ya jengo,”anasema Bw Njeru.

Hoteli hiyo iliyoanzisha mnamo 1948, inamiliki matawi mengine 25 duniani.

Ndani ya hoteli ya DusitD2, kuna mashirika mengine makubwa kama vile Reckitt Benckiser, Amadeus Global Travel Distribution Ltd, Colgate Palmolive (EA) Limited and Cellulant Kenya Limited.

Kampuni nyingine zenye afisi katika hoteli hiyo ni Brighter Monday Limited, Pernod Ricard, Metta, LG, Redhouse PR, Fanisi Capital, Nielsen, Secret Garden Café, Amadiva Salon, Visa, CRA, Deepa Dosaja, na benki ya I&M.