Makala

Sababu za fisi kugeuza watu kuwa kitoweo

Na FRIDAH OKACHI August 29th, 2024 2 min read

HUKU matukio ya fisi kuvamia binadamu katika eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu na Kaunti ya Vihiga, yakizidi kuongezeka, imeibuka ni watu wanaowavutia kutoka mwituni.  

Mwanasayansi na pia Mkurugenzi katika Kituo cha Elephant Neighbors, Dkt Jim Justus Nyamu alisema upungufu wa mizoga kwenye misitu, umechangia pakubwa fisi hao kupatikana karibu na makazi ya binadamu kutokana na mabadiliko ya mazingira.

“Makao ya fisi ni msitu na hutegemea mizoga ya wanyama wanaouawa na simba au chui. Mizoga hiyo imepungua. Fisi analazimika kuingia katika maeneo ya binadamu kutafuta chakula na makazi,” alieleza Bw Nyamu.

Aliongeza kuwa hali hiyo imechangiwa pakubwa na uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za kibinadamu ambazo ni ukataji miti, kilimo na ujenzi wa miundombinu.

Alitaja ongezeko la idadi ya watu na upanuzi wa makazi ya binadamu katika maeneo ya karibu na misitu na hifadhi za wanyama kuwa tatizo kuu. Watu wanapozidi kuvamia maeneo ya pori kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, wanapunguza mipaka ya wanyama hawa kuishi, na hivyo kusababisha mwingiliano kati ya fisi na binadamu.

Akirejelea visa vya fisi kugeuza binadamu kuwa kitoweo katika eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu mwezi Julai 2024 na Januari 2024, Bw Nyamu alisema baadhi ya wakazi, wafugaji nchini wamepuuzilia mbali kuchanja wanyama wao ambao hufariki na kuwatupa ovyoovyo.

Bw Jim Justus Nyamu baada ya mahojiano na Taifa Dijitali jijini Nairobi. PICHA|FRIDAH OKACHI

“Idadi kubwa ya kuku na mbwa, hawapati chanjo na kuchangia wao kufariki. Mkulima au mmiliki wa wanyama hao huwatupa bila kuwazika. Harufu ya mizoga ya wanyama hao hufuatwa na fisi,” alidokeza mhifadhi huyo.

Alipendekeza wizara husika na wananchi ambao wanafuga wanyama hao kuzingatia chanjo.

“Fisi hafai kula watu. Lakini fisi akila mzoga wa paka au mbwa aliye na kichaa, pia anapatwa na kichaa cha kumuuma binadamu ovyoovyo,” alifafanua.

Jumatano asubuhi, Agosti 28, 2024, maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Vihiga walichukua vipande vya mwili, unaoaminika kuwa wa mtu aliyetafunwa na fisi katika eneo la Gambogi.

Afisa wa polisi aliyezungumza na Taifa Dijitali, alisema visa vya fisi kula binadamu eneo hilo vimeongezeka.

“Nimekuwa miongoni mwa maafisa ambao hukusanya miili iliyoliwa na fisi Kaunti ya Vihiga. Msitu wa Maragoli Hills sio msitu tena wa kuhifadhi wanyama hao ambao wanajificha kwa makazi ya watu,” alisema afisa huyo.