Michezo

Sababu za FKF kumtimua Kimanzi na kumteua Mulee

October 22nd, 2020 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

SABABU za Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kumtema kocha Francis Kimanzi na mikoba aliyokuwa akiidhibiti kambini mwa Harambee Stars kutwaliwa na Jacob ‘Ghost’ Mulee, zimefichuka.

Kimanzi na waliokuwa wenzake kwenye benchi ya kiufundi ya Stars – Zedekiah ‘Zico’ Otieno na Lawrence Webo – waliagana na FKF mnamo Jumanne, siku chache kabla ya timu ya taifa ya Stars kushuka dimbani kuvaana na Comoros kwenye mechi mbili za Kundi G za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

Baada ya kupepetana na Comoros kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Novemba 11 jijini Nairobi, Stars watarudiana na wanavisiwa hao jijini Moroni mnamo Novemba 15.

Japo Kimanzi ameshikilia kwamba hajui kiini cha kutimuliwa kwake, Taifa Leo imebaini kwamba uhusiano kati ya mkufunzi huyo na usimamizi wa FKF ulikuwa mbaya.

Japo Zico na Webo hawakuwahi kuvurugana na uongozi wa FKF, wawili hao walijipata katika ulazima wa kusombwa na mawimbi yaliyompata Kimanzi.

“Hakuna jinsi ambavyo kocha mkuu angepigwa kalamu na wasaidizi wake wasalie,” akasema mdokezi wetu kwa kusisitiza kwamba huenda Rais Nick Mwendwa akawapa wawili hao majukumu mengine baadaye katika makao makuu ya shirikisho; Kandanda House.

Kwa mujibu wa mdokezi huyo ambaye alitaka jina lake libanwe, inaaminika kwamba Kimanzi alilalamikia suala la kucheleweshwa kwa marupurupu ya wachezaji wa Stars kabla ya kikosi hicho kuvaana na Chipolopolo ya Zambia kwenye mechi ya kirafiki iliyowakutanisha ugani Nyayo, Nairobi mnamo Oktoba 9.

“Ililazimu mtafaruku huo kuingiliwa kati na nahodha mshikilizi Brian Mandela aliyejaribu kupatanisha Mwendwa na Kimanzi aliyelalamikia jinsi FKF ilivyokuwa ikitumia fedha nyingi kwa minajili ya kampeni za uchaguzi mpya uliofanyika Oktoba 17 badala ya kulipa marupurupu ya kikosi cha Stars kwa wakati,” akasema mdokezi.

“Suala hilo lilichukuliwa kwa uzito na maafisa wakuu wa FKF ambao hawakufurahishwa kabisa na mtazamo wa Kimanzi kuhusu baadhi ya mambo. Zico na Webo ni watu wetu na shirikisho litawapa hifadhi,” akaongeza.

Inaaminika kwamba uhusiano kati ya Kimanzi na FKF uliingia mdudu kuanzia Disemba 2019 wakati wa fainali za kipute cha Baraza la Mashirikisho ya Soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) nchini Uganda.

Wakati huo, Kimanzi alitaka Stars wasusie mechi ya ufunguzi dhidi ya Tanzania huku akilalamikia hatua ya wapinzani wao hao kupanga kikosini wanasoka waliokosa stakabadhi muhimu na vibali ‘halali’ vya kusafiri hadi Uganda.

Licha ya kuchelewa kuanza, mechi hiyo iliyokuwa ikipeperushwa moja kwa moja runingani iliendelea baada ya Mwendwa kupiga simu kwa waandalizi kutoka Nairobi. Kutokana na mtafaruku huo uliofasiriwa kuwa utovu wa nidhamu na ukosefu wa sifa za uanaspoti, Kimanzi alipigwa marufuku ya mechi mbili zilizosimamiwa na Zico dhidi ya Sudan (2-1) na Zanzibar (1-0).

Afisa mwingine wa FKF amedai kwamba Kimanzi ni mtu aliyekuwa na misimamo mikali na aghalabu alikwaruzana na vinara wa FKF kuhusu uteuzi wa wachezaji wa kuunga kikosi cha Stars.

“Kimanzi hakukubali presha ya kupangiwa kikosi au kupendekezewa baadhi ya wachezaji wa kuunga kikosi chake. Hiyo huenda ikawa ni sababu nyingine ya kutimuliwa kwake kabla ya mkataba aliokuwa nao kukamilika,” akasema.

Kwa upande wake, Kimanzi amesema: “Najivunia matokeo bora ambayo Stars walisajili chini yangu. Nimeagana na kikosi kikiwa thabiti zaidi kuliko jinsi nilivyokipata. Mengi yamesemwa na yatasemwa.”

Mbali na kutoonekana kumuunga Mwendwa mkono katika kampeni zake za kuchaguliwa kuhudumu kwenye kiti cha urais wa FKF kwa awamu ya pili ya miaka minne, zipo sababu tele ambazo wadau wamehusisha na kutemwa kwa Kimanzi kisha kuteuliwa kwa Mulee.

Mwenyekiti wa Kakamega Homeboyz, Cleophas Shimanyula amedai kwamba Kimanzi alikuwa akitoa nje siri za FKF na kwa wakati fulani, Mwendwa alikuwa amefichua maazimio ya kumtimua na kumpokeza mikoba Adel Amrouche aliyewahi kunoa Stars (2013-14).

“Yasikitisha kwamba Kimanzi ametimuliwa na FKF wakati ambapo kikosi cha Stars kilikuwa kinajivunia ufufuo mkubwa na kuonyesha dalili zote za kufuzu kwa fainali za AFCON 2021 na Kombe la Dunia 2022,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Nairobi City Stars, Patrick Korir katika mawazo yaliyoungwa mkono na beki wa zamani wa kimataifa, James Situma.

“Sijui kiini cha kutemwa kwa Kimanzi, lakini hatua hiyo ya FKF ni pigo kubwa kwa timu ya taifa. Hata hivyo, Mulee ambaye ni mrithi wa Kimanzi pia ana tajriba ya kutosha na amewahi kudhirisha sifa za kuhusiana vyema na wachezaji na wakufunzi wa vikosi vya ligi mbalimbali za humu nchini,” akasema Mwenyekiti wa Chama cha Makocha nchini Kenya, Bob Oyugi.

Hata hivyo, mdokezi wetu kutoka Kandanda House amesema kwamba kuteuliwa kwa Mulee, sawa na kulivyowahi kufanyika kwa Okumbi, ni msukumo wa Mwendwa ‘kutuza’ washirika wake wa karibu ambao ni wepesi wa kumuunga mkono katika mengi ya maamuzi na mipango binafsi.

“Tumtarajie pia kocha William Muluya ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya kikosi cha Kariobangi Sharks kinachomilikiwa na Mwendwa kwenye benchi ya kiufundi ya Stars,” akatanguliza kwa kufichua kuwa Mulee alikuwa na ushawishi mkubwa kwenye dili ya FKF na StarTimes.

Wakati wa kuzinduliwa kwa BetKing watakaodhamini Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL) kwa miaka mitano ijayo kwa kima cha Sh1.2 bilioni, Mwendwa alifichua mipango ya FKF kushirikiana na kampuni ya StarTimes ambayo sasa itapeperusha baadhi ya mechi za ligi hiyo moja kwa moja kwa miaka saba ijayo.

Maafikiano hayo kati ya FKF na StarTimes yatashuhudia vikosi vyote 18 vya Ligi Kuu ambavyo tayari vina uhakika wa kupokezwa Sh8 milioni kutoka BetKing kila msimu, sasa vikipigwa jezi zaidi kifedha. FKF imewahakikishia wadau wa soka ya humu nchini kwamba klabu za Ligi Kuu sasa zitakuwa zikipokea jumla ya Sh12 milioni kila msimu kwa kuwa StarTimes watakuwa wakitoa Sh4 milioni zaidi kwa kila kikosi.

Mulee kwa sasa anatarajiwa kuongoza Stars kufuzu kwa fainali za AFCON 2021 nchini Cameroon na fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini Qatar mnamo 2022. Kenya imepangwa na Mali, Rwanda na Uganda katika Kundi E kwenye gozi la kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Qatar. Wako katika Kundi B kwa pamoja na Comoros, Togo na mabingwa mara saba, Misri kwenye AFCON.

Chini ya Kimanzi ambaye pia amewahi kuwanoa Mathare United (2002-10; 2015-19), Sofapaka (2011) na Tusker (2013-15), Stars walianza kampeni zao za kufuzu kwa fainali za AFCON 2021 dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14, 2019 ugenini kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18, 2019 jijini Nairobi.