Makala

Sababu za kilimo cha mboga kuwa ghali

January 19th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

MBOGA ni chaguo la chakula katika maboma mengi Kenya, ambacho kinachangia pakubwa kuangazia uhaba wa lishe na kero ya utapiamlo. 

Hata hivyo, kiwango cha usambazaji wa kiungo hiki kilichosheheni Vitamini kingali chini kwa sababu ya changamoto za uzalishaji.

Kisababishi kikuu cha gapu hii ni kuendelea kutozwa ushuru (VAT) kwa mbegu, hivyo basi kuathiri ukuzaji.

Kampuni na mashirika yanayozalisha mbegu za mboga yanapendekeza kuondolewa ushuru.

Muungano wa Wazalishaji Mbegu Kenya (STAK), shirika linaloleta pamoja kampuni za kibinafsi na umma, linasema kuendelea kutoza ushuru mbegu za mboga kunalemaza uzalishaji.

VAT ya juu inafanya mbegu kuwa ghali, kilele kikiwa uzalishaji kuathirika.

Wafanyakazi wa Kampuni ya Royal Seed wakionyesha mbegu za mboga zilizopakiwa wakati wa Maonyesho ya STAK Mazao. PICHA|SAMMY WAWERU

Wellington Wasike, Mwenyekiti STAK, anaainisha athari za ushuru wa juu, akisema, “Wakulima wanaishia kukosa bidhaa hii muhimu, na kuendeleza kutoza mbegu VAT kunachochea gharama ya uzalishaji kupanda mara dufu. Suluhu ya changamoto hii inayotishia ajenda kuu kuangazia uhaba wa chakula nchini, tunahimiza serikali kuondoa ushuru na ada za juu kwa mbegu”.

STAK, imesajiliwa kupitia Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis), na imekuwa ikisukuma serikali kuondoa au kupunguza VAT ya mbegu za mboga.

Huku shirika hilo likiendelea kutetea wanachama wake, jitihada zake kuletea wakulima afueni hazijazaa matunda.

Kwa mujibu wa data za ukuaji wa uchumi nchini 2023 za Shirika la Takwimu Kenya (KNBS), kiwango cha mboga zilizouzwa ng’ambo kimeshuka.

Kati ya Januari na Februari 2023, kiwango cha mboga zilizouzwa nje ya nchi kilishuka kutoka tani metri (MT) 8,336.23 hadi 5,751.40 MT.


Mkulima na mteja wake wakivuna mboga aina ya spinachi. PICHA|SAMMY WAWERU

Mapato nayo yalipungua kutoka Sh1,947.72 milioni hadi Sh 1,576.61 milioni kipindi hicho, mshuko unaopaswa kugutusha serikali.

Sekta ya uzalishaji mboga, Wasike anaamini inaweza kuwa kitega uchumi kikuu na kubuni nafasi chungu nzima za ajir, ikiwa VAT ya mbegu itaondolewa.

Anasisitiza, “Hata ingawa ushuru ni nguzo kuu katika uboreshaji uchumi, mboga zinachangia pakubwa katika kuangazia usalama wa chakula na kilimo chake ni sekta inayoweza kuzika katika kaburi la sahau ukosefu wa kazi hasa kwa vijana”.

STAK imekuwa ikiandaa makongamano kila mwaka kuleta pamoja wadauhusika kutoka asasi za umma – serikali, na kibinafsi, na mwishoni mwa 2023 muungano huo uliandaa kongamano katika makao makuu ya Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro), ambapo washirika walihimiza haja ya kusawazisha VAT na kuinua sekta ya kilimo ambayo ni nguzo kuu katika ukuaji wa nchi.

Maboma mengi hasa kwenye mabustani yake yanaweza kuzalisha mboga kwa kiwango kikubwa, ila gharama ya mbegu halisi na zilizoidhinishwa na Kephis inawalemea.

Ukumbatiaji mifumo ya kisasa, kama vile “mashamba ya ghorofa yaliyoundwa kwa kutumia mifereji ya plastiki”, PVC, maeneo ya mijini yakitumika uhaba wa mboga utaangaziwa pakubwa.

Kando na kuzalisha mboga, bunifu hiyo pia inaweza kutumika kukuza mseto wa mboga na viungo vya mapishi.

Leonard Kubok, Naibu Mkurugenzi wa Malighafi na Usimamizi wa Mazao katika Wizara ya Kilimo na Mifugo, anasema serikali inafanya juhudi kuona gapu ya uzalishaji mboga nchini inaangaziwa.

Wakulima wakiwa katika makao makuu ya KALRO wakihamasishwa umuhimu wa kununua mbegu zilizoidhinishwa na KEPHIS. PICHA|SAMMY WAWERU

Afisa huyu anadokeza kwamba utafiti unaohusisha matumizi ya sehemu za mimea inayozalishwa kwa njia ya kujitokeza, kama vile shina, majani, au mizizi, ili kuendeleza mimea ya wazazi unaendelea kwa minajili ya uwepo wa njia endelevu ya uzalishaji.

“Serikali imejitolea kutatua suala la usalama wa chakula na utapiamlo, na inatathmini kupiga jeki sekta ya mboga,” Kubok anasisitiza.

Hali kadhalika, STAK kwa ushirikiano na asasi husika inaendelea kufanya mazungumzo na Baraza la Magavana Nchini (CoG) ili kuondoa ada zinazotozwa usafirishaji pembejeo na mazao ya shambani katika boda ya kila kaunti.

Afisa Mkuu Mtendaji STAK, Duncan Onduu kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali Dijitali alisema kila kaunti ina malipo yake.

“Ada hizo, maarufu kama Cess zimechochea gharama ya pembejeo na hata chakula kuwa ghali,” akasema.

Muungano huo unapendekeza kuwe na ada moja.