Sababu za kudhibiti filamu wanazotazama watoto

Sababu za kudhibiti filamu wanazotazama watoto

Na SAMMY WAWERU

Ni jambo la kuhuzunisha familia kupoteza watu watano kwa wakati mmoja, kupitia kitendo cha ukatili. Juma lililopita, taifa lilishtushwa na taarifa ya mvulana anayeshukiwa kuua babake, mamake, kaka yake na binamu pamoja na mfanyakazi katika Kaunti ya Kiambu.

Huku Idara ya Uchunguzi wa Jinai na Uhalifu (DCI) ikiendeleza uchunguzi baada ya mshukiwa huyo mkuu kufunguliwa mashtaka mahakamani, Lawrence Warunge, 22, alikiri kushawishiwa na filamu ya Kibritania (British) kutekeleza mauaji hayo ya kinyama.

Akikiri kutekeleza mauaji, kijana Warunge na ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha MKU, alieleza maafisa wa DCI kwamba filamu ‘Killing Eve’ ilimchochea kuondoa uhai wa jamaa zake.

Ni kisa cha kuhuzunisha na kinachopaswa kuwa mwamko wa wazazi na taifa kwa jumla kufahamu kwa kina filamu na michezo ya kuigiza inayopeperushwa kwenye runinga na pia kupakiwa mitandaoni.

Warunge kukiri filamu hiyo potovu kimaadili na kimatendo kwa watoto na vijana wetu, ilimchochea kuua wanafamilia ni jambo linalopaswa kututia wasiwasi, wasiwasi mkubwa mawazo ya watoto wetu yakitekwa bakunja na ‘maisha na tabia za ughaibuni’.

Kitendo hicho kiwe mwamko, wazazi wawe makini wanachotazama wanao.

Isemwavyo, udongo uwahi ukiwa maji na pia samaki mkunje akiwa angali mbichi, maisha ya baadaye ya watoto na vijana yanategemea msingi wa malezi hasa wakiwa wangali wadogo kiumri.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kukagua Filamu Nchini (KFCB), Dkt Ezekiel Mutua amekuwa akikariri mara kwa mara haja ya runninga kuchuja filamu zinazopeperushwa.

Huku baadhi ya wakosoaji wake wakimsuta kutokana na msimamo wake mkali, Dkt Mutua amekuwa akiweka wazi mmomonyoko wa kimaadili na nidhamu unaoshuhudiwa miongoni mwa watoto wetu na vijana unachangiwa na wanachotazama kwenye runinga na pia machapisho mitandaoni, video na picha zinazopakiwa.

“Tunaposema kinachotazamwa na watoto wetu kinachangia kudorora kwa usalama wa kitaifa, tukio kama hili (Lawrence Warunge kukiri kuchochewa na filamu potovu kuua jamaa zake) ndilo tunamaanisha.

“Baadhi ya yanayopeperushwa na vyombo vya habari yanachangia kuathiri tabia na fikra za wateja, hususan watoto. Watoto wanaotazama filamu za kivita huishia kushiriki vita mara kwa mara wanapokomaa,” Dkt Mutua anaelezea.

Akionya vyombo vya habari, Afisa huyo Mkuu wa KFCB anasema matangazo mengi ya vyombo vya habari hasa vituo vinavyolipiwa ada, yanasifia vita na uhalifu, dawa za kulevya, ngono, ubakaji na lugha chafu.

“Wazazi hulipia ada watoto kutazama vituo hivyo bila kujua programu zinazopeperushwa. Hatimaye wanapotoka kimaadili machoni pao,” Dkt Mutua anasema, akionya tahadhari isipochukuliwa huenda maadili ya vijana yakageuzwa na filamu wanazotazama.

“Umewadia wakati tukaze kamba sheria kudhibiti yanayopeperushwa katika vyombo vya habari.”

Kwa hakika kauli na msimamo wa Dkt Mutua ni bayana na yenye ukweli, hasa unapotazama watoto mitaani wakicheza, baadhi utawaona wakiwa na vifaa vya kuchezea vyenye muundo wa bastola au bunduki.

Wakiiga wanayotazama kwenye filamu, utawaona wakifyatulia wenzao ‘risasi’, ishara ya kushawishiwa na program hizo hatari.

Ili maji yasizidi unga, kisa cha mauaji ya Kiambu kiwe mwamko kwa wazazi na vyombo vya habari yanayopeperushwa yadhibitiwe.

Teknolojia inavyozidi kuimarika kila uchao, ni muhimu kufahamu ina mchango mkubwa katika malezi ya watoto na vijana, ambao ni wazazi na viongozi wa kesho.

Kwa hakika, wanahitaji malezi bora na yenye uadilifu wa hali ya juu ili wawe kielelezo katika jamii na kwa vizazi vijavyo.

You can share this post!

DINI: Fursa hubisha hodi mara moja, ikumbatie

Hatimaye Ozil aondoka Arsenal