Michezo

Sababu za kushuhudiwa kwa idadi kubwa zaidi ya mabao katika EPL hadi kufikia sasa msimu huu wa 2020-21

October 7th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUTOKUWEPO kwa mashabiki uwanjani ni miongoni mwa sababu ambazo zimetolewa kuwa kiini cha idadi kubwa ya mabao yanayoshuhudiwa kwa sasa katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2020-21.

Katika wikendi ya Oktoba 3-4, 2020 pekee, jumla ya mabao 41 yalishuhudiwa katika mechi 10 za EPL huku mechi iliyokutanisha Aston Villa na Liverpool pekee ikizalisha jumla ya magoli tisa baada ya Villa kuzamisha chombo cha mabingwa hao watetezi kwa kichapo cha 7-2.

Mechi nyingine iliyoshuhudia idadi kubwa zaidi ya magoli ni ile iliyowakutanisha Tottenham Hotspur na Manchester United. Kocha Jose Mourinho aliwaongoza masogora wake wa Spurs kuwapepeta Man-United 6-1 ugani Old Trafford.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 90, mvua kubwa zaidi ya mabao inashuhudiwa katika soka ya EPL. Katika mechi 38 za ufunguzi wa msimu huu wa 2020-21, jumla ya magoli 144 yamefungwa. Idadi hii ina mabao 40 zaidi kuliko kiasi kilichoshuhudiwa katika mechi 38 za kwanza katika muhula uliopita wa 2019-20.

Ina maana kwamba idadi wastani ya mabao ambayo yamekuwa yakifungwa katika EPL ni 3.79 kwa kila mechi – hii ikiwa kiasi kikubwa zaidi cha magoli katika EPL tangu kiwango wastani cha mabao 3.95 kwa mechi kishuhudiwa mnamo 1930-31.

Mechi 11 kati ya 38 za hadi sasa msimu huu zimeshuhudia angalau jumla ya mabao matano yakifungwa (asilimia 29). Hiyo ndiyo asilimia kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika msimu mmoja tangu 1960-61.

Mnamo Oktoba 4, 2020, Liverpool waliweka historia ya kuwa mabingwa watetezi wa kwanza wa EPL baada ya Arsenal mnamo 1953 kuokota wavuni jumla ya mabao saba katika mechi moja.

Hata hivyo, idadi ya mipira inayolenga shabaha kwenye malango ya wapinzani imepungua pakubwa japo uhakika wa kufungwa kwa mabao kumeongezeka hadi asilimia 16.1 kutoka asilimia 11 msimu uliopita wa 2019-20.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mlinzi wa kimataifa wa Everton na timu ya taifa ya Uingereza, Michael Keane, zipo sababu mbalimbali zinazozidi kuchangia idadi kubwa ya mabao katika EPL kwa sasa.

Keane amesema ni kawaida mno kwa timu kufungwa mabao matatu, na baadaye kumaliza mechi kwa ushindi wa 4-3 au 5-3.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 27 alisema sababu nyingine inayochangia mabadiliko haya ni sheria ngumu za kutenganisha wachezaji kwa lengo la kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Alisema wachezaji wamepata uhuru wa kujaribu mbinu kadhaa ambazo wasingeweza Kujaribu wanapoangaliwa na mashabiki uwanjani.

“Wachezaji wamezoea mashabiki kuwapa motisha ya kucheza na ari ya kujituma zaidi ila kwa kujizuia sana kufanya makossa ambayo yatachochea lawama,” akaongeza beki huyo.

“Nimezungmza na baadhi ya wachezaji wa kriketi pamoja na wanamichezo wengine ambao wamewahi kucheza bila uwepo wa mashabiki ambao wamesema ni wachezaji wengi hutia bidii wanapocheza mbele ya mashabiki.”

Alan Shearer na Jermain Jenas ni miongoni mwa wanasoka wa zamani waliounga mkono maoni hayo huku wakidai kwamba inakuwa vigumu kwa masogora kujitahidi wanapocheza bila mashabiki uwanjani.

Jenas alisema alisema baadhi ya marefa pia wamepata fursa za kutoa uamuzi usiofaa kwa sababu hawawezi kofokewa na mashabiki hadharani sawa na jinsi hali ilivyokuwa hapo awali.

Kutokana na vizuizi vilivyowekwa, wachezaji wamekuwa pia wakijiandaa wanavyotaka bila ya kudhibitiwa vilivyo na wakuu wao kambini.

Kocha Carlos Carvalhal wa klabu ya Braga nchini Ureno na aliyekuwa kocha wa klabu ya Sheffield Wednesday na Swansea City alisema: “Klabu kubwa zinazoea kucheza mbele ya mashabiki wengi ambao huwasukama wajitahidi zaidi. Mashabiki wanapanua mawanda ya fikira za mchezaji na kufanya ajaribu mbinu mbadala za kuwapiku wapinzani. Hali hiyo huzidisha viwango vya ushindani na kuzua uoga kwa timu pinzani uwanjani.”

Aliyekuwa mshambuliaji matata wa timu ya taifa ya Uingereza, Chris Sutton amedai kwamba kukosekana kwa mashabiki kumefanya idadi kubwa ya washambuliaji kushindwa pia kufunga mabao huku makipa wakiwa sasa wepesi wa kuachilia mipira kutikisa nyavu zao kirahisi.

Mbali na kukosekana kwa mashabiki, sababu nyinginezo ambazo Sutton anasema zinachangia idadi kubwa ya mabao katika EPL kwa sasa ni masihra ya baadhi ya wachezaji, uchovu, mavune, ukosefu wa maandalizi ya kutosha na kutumiwa sana kwa teknolojia ya VAR kufanyia maamuzi mbalimbali.