Michezo

Sababu za Olunga kukosa mechi nne zijazo za Harambee Stars

September 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SASA ni rasmi kwamba mfumaji Michael Olunga atakosa mechi nne zijazo za Harambee Stars, zikiwemo mbili dhidi ya Comoros katika juhudi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zitakazoandaliwa Cameroon mnamo 2021.

Chini ya kocha Francis Kimanzi, Stars wamepangiwa kuvaana na Comoros katika mkondo wa kwanza jijini Nairobi mnamo Novemba 9 kabla ya kurudiana na kikosi hicho jijini Moroni siku nne baadaye.

Kabla ya kupigwa kwa mechi hizo za mikondo miwili dhidi ya Comoros katika Kundi G linalojumuisha pia Togo na Misri, Stars wameratibiwa kupimana nguvu na Zambia na Sudan mwezi ujao.

Ingawa hivyo, Kashiwa Reysol wanaojivunia huduma za Olunga katika Ligi Kuu ya Japan (J1-League), wamethibitisha kwamba hawatamwachilia fowadi huyo kurejea Kenya kuwajibikia Stars kwa sasa.

Iwapo atatua humu nchini kuchezea Stars, Olunga atalazimika kukosa jumla ya michuano saba ya Kashiwa kwa sababu ya kanuni za afya zinazodhibiti msambao wa ugonjwa wa Covid-19.

“Japan wana masharti makali ya kukabiliana na janga la corona. Haitakuwa rahisi kwa Olunga kuchezea Kenya katika mechi mbili zijazo za kufuzu kwa AFCON dhidi ya Comoros,” ikasema sehemu ya taarifa.

Iwapo Kashiwa watamwachilia Olunga, nyota huyo anayehofia kushuka kwa fomu yake atalazimika kuingia karantini kwa siku 14 kabla ya kuruhusiwa tena kuchezea waajiri wake ambao kwa kipindi hicho watakuwa na mechi muhimu ligini.

“Nilianza vyema kampeni za msimu huu wa 2020 kabla ya corona kubisha. Ligi iliporejelewa baada ya miezi minne, nilitatizika sana kufunga mabao katika mechi tatu za kwanza. Nilijinyanyua baadaye na kutikisa nyavu za wapinzani mara saba mfululizo,” akasema Olunga.

Kufikia sasa, Olunga ambaye pia amewahi kuchezea Thika United, Tusker na Gor Mahia katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL), anaongoza orodha ya wafungaji bora wa J1-League kwa mabao 16 kutokana na mechi 18.

Mbali na shaka kuhusu uwezekano wa kujivunia huduma za masogora wote wanaosakatia klabu za ughaibuni, Kimanzi anahofia pia namna ya kuandaa wachezaji wa ligi za humu nchini kwa minajili ya vibarua vinne vijavyo vya Stars kutokana na ukali wa kanuni za Wizara ya Michezo.

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limetaka Wizara ya Michezo kuidhinisha kurejelewa kwa mchezo wa soka humu nchini.

“Kenya imepangiwa kushiriki mechi za kupimana nguvu mwezi ujao. Tunahitaji kujiandaa vilivyo. Tumeomba Wizara ya Michezo itukubalie kuita wachezaji kambini na kuanza kujifua kwa wakati ufaao,” akatanguliza Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno.

“Gor Mahia pia wana kibarua katika soka ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) na tunahitaji kupata mshindi wa FKF Shield Cup ili tuwe na mwakilishi wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Conferations Cup) msimu ujao wa 2020-21. Katika barua yetu kwa Wizara ya Michezo, tumeahidi kuhakikisha kuwa wadau wote wanazingatia kanuni zilizopo za afya kuhusu Covid-19,” akaongeza Otieno.

FKF imeandikia pia klabu zinazojivunia huduma za wanasoka wa Stars katika mataifa ya nje ziwe radhi kuwaachilia wachezaji hao kusafiri humu nchini pindi Kimanzi atakapowaita kambini.

Kati ya masogora ambao Kimanzi anatazamiwa kutegemea katika vipute vijavyo vya Stars ni beki wa kushoto wa Barnsley ya Uingereza, Clarke Oduor.

Stars kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi G la kufuzu kwa fainali za AFCON 2021. Wanajivunia alama mbili kutokana na sare za 1-1 dhidi ya Misri mnamo Novemba 14, 2019 (ugenini) kisha na Togo mnamo Novemba 19, 2019 (nyumbani) katika mechi mbili za ufunguzi wa Kundi G.