KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Qatar yadenguliwa baada ya kuchapwa na Senegal 3-1 na mechi kati ya Ecuador na Uholanzi kukamilika kwa sare ya 1-1

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Qatar yadenguliwa baada ya kuchapwa na Senegal 3-1 na mechi kati ya Ecuador na Uholanzi kukamilika kwa sare ya 1-1

Na MASHIRIKA

WENYEJI Qatar walikuwa wa kwanza kuaga fainali za Kombe la Dunia mwaka huu baada ya Senegal kuwapokeza kichapo cha 3-1 ugani Al-Thumama nao Ecuador kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Uholanzi katika mechi za pili za Kundi A mnamo Novemba 25, 2022.

Qatar ndilo taifa la kwanza kutoka Mashariki ya Kati kuwahi kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia. Mabingwa hao wa Asian Cup walifungua kampeni za Kundi A kwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Ecuador mnamo Novemba 20 ugani Al Bayt, siku moja kabla ya Uholanzi kutandika Senegal 2-0 uwanjani Al-Thumama.

Licha ya Qatar kubanduliwa, kocha Felix Sanchez amesisitiza kwamba matokeo ya kikosi chake hayapaswi kutajwa kuwa ya kusikitisha kwa kuwa vijana wake walijituma kadri ya uwezo wao.

Sasa Kundi A liko wazi kwa vikosi vitatu – Senegal, Uholanzi na Ecuador – kuwania nafasi ya kutinga hatua ya 16-bora. Hata hivyo, pambano kati ya Senegal na Ecuador linatarajiwa kuwa la kufa-kupona huku Uholanzi wakipigiwa upatu wa kutandika Qatar katika pambano la mwisho la Kundi A.

Qatar sasa ndilo taifa la pili baada ya Afrika Kusini mnamo 2010 kuaga fainali za Kombe la Dunia katika hatua ya makundi likiwa mwenyeji.

Walihitaji hisani kubwa ya Ecuador kutandika Uholanzi ili kuweka hai matumaini ya kusalia kwenye kipute hicho cha mwaka huu. Bao la Qatar dhidi ya Senegal lilifumwa wavuni na Mohammed Muntari huku Senegal ambao ni mabingwa wa Afrika wakipata magoli yao kupitia kwa Boulaye Dia, Famara Diedhiou na Bamba Dieng.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Vinara wakuu Azimio washutumu Kenya Kwanza kwa kulipiza...

Mama wa kambo alinifinya nyeti, mwanaume alilia korti

T L