Sababu za Rais ‘kuhepa’ mkutano wa Raila- Wadadisi

Sababu za Rais ‘kuhepa’ mkutano wa Raila- Wadadisi

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kutohudhuria mkutano wa leo ambapo kiongozi wa ODM Raila Odinga anatangaza rasmi azma yake ya kuwania urais 2022, imeibua hisia mseto.

Kuna wadadisi ambao wanahisi kwamba hatua hiyo imeonyesha kuwa Rais Kenyatta anaheshimu nafasi yake kikatiba kama nembo ya umoja wa taifa.Hii ni licha ya kwamba kiongozi wa taifa ameonyesha dalili kwamba Bw Odinga ndiye chaguo lake katika kinyang’anyiro cha urais baada ya kutofautiana kisiasa na naibu wake, William Ruto.

“Sidhani kama Rais Kenyatta angehudhuria mkutano wa Azimio la Umoja kule Kasarani hata kama angekuwa nchini. Bado ni mapema kwake kuonyesha wazi wazi kwamba amemwidhinisha Raila. Wakati huu bado anafaa kuonekana kama ishara ya umoja wa taifa, “ mchanganuzi wa kisiasa, Bw Martin Andati akasema.

Rais yuko nchini Tanzania kwa ziara rasmi iliyoanza jana alipohudhuria sherehe ya kuadhimisha miaka 60 tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake.Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Bw Dan Kazungu alisema leo Rais Kenyatta na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu, wanatarajiwa kutia saini mikataba minane ya makubaliano kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo biashara.

Wafuasi wa Rais Kenyatta katika ngome yake ya Mlima Kenya na wale wa Bw Odinga walikuwa na matumaini makubwa kwamba angehudhuria mkutano wa leo ambao ulitajwa kama kilele cha maridhiano kati yake na Bw Odinga.

Japo, Rais hatafika katika mkutano huo duru ziliambia Taifa Leo kwamba mawaziri kadhaa waaminifu kwake na wabunge wa chama chake cha Jubilee wamethibitisha kuwa watafika Kasarani. Kulingana na Bw Mark Bichachi, hii ni ishara tosha kwamba Bw Odinga ndiye chaguo lake miongoni mwa wagombeaji wote wa urais.

“Ikumbukwe kwamba Rais Kenyatta amekuwa akitumia lugha ya mafumbo kumpigia debe Raila jinsi alivyofanya juzi mjini Nakuru. Isitoshe, kiongozi huyu wa ODM amekuwa akipata usaidizi kutoka kwa asasi za serikali za usalama,” akaeleza.

You can share this post!

Azimio la Umoja kumeza Jubilee, ODM

TAHARIRI: Dereva, abiria washirikiane kuzuia ajali msimu huu

T L