Habari za Kitaifa

Sababu za seneti kutaka korti kuondoa agizo la kusitisha kutimuliwa kwa Mwangaza


SENETI inataka agizo la Mahakama Kuu la kusitisha kutimuliwa mamlakani kwa Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza, liondolewe.

Katika majibu yake ya kesi iliyowasilishwa na Bi Mwangaza katika Mahakama Kuu, Nairobi, Seneti inasema kuwa Bi Mwangaza alimshtaki Spika wa Bunge hilo Amason Kingi na kuwaacha nje maseneta waliopiga kura kuunga mkono kuondolewa kwake ofisini.

Maseneta wanaotaka kujiunga na kesi hiyo waliteta kuwa ni Seneti pekee inayoweza kujibu masuala yaliyoibuliwa kwenye mchakato wa kumuondoa Gavana Mwangaza.

“Kwa hivyo, kuachwa kwa Seneti ya Jamhuri ya Kenya katika kesi hii kunaifanya kuwa na dosari isiyoweza kurekebika,” maseneta wanaeleza korti.

Zaidi ya hayo, Seneti ilisema mahakama ilitoa muda wa wazi bila dalili kuhusu ni lini uamuzi wa kesi utatolewa au hata wakati kesi itasikizwa.

Maseneta hao walisema agizo hilo lililotolewa Agosti 21, 2024 linakiuka kanuni za haki , ambazo zinaeleza kwamba wahusika wana haki ya kusikilizwa kabla ya amri kutolewa dhidi yao.

“Seneti haikupewa fursa ya kusikilizwa,” Bw Kingi alisema akijibu kesi.