Bambika

Sababu za wengi mashambani kumwagia Valentino maji baridi

February 17th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

LICHA ya Siku ya Valentino kuzua hisia na msisimko wa aina yake mnamo Jumatano miongoni mwa Wakenya, wakazi wengi katika maeneo ya mashambani waliendelea na shughuli zao kama kawaida.

Wengi waliitaja siku hiyo kuwa “utamaduni wa Wazungu unaolenga kuwaharibu Waafrika”.

Wengine waliitaja kama “ya vijana au watu wa mijini”, huku wengine wakionekana kutoitambua hata kidogo.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika maeneo mengi ya mashambani ulibaini kwamba watu wengi walikuwa wakiendelea na shughuli zao, wengine hata bila kufahamu uwepo wa siku hiyo.

Katika soko la Mairo Inya, lililo katika Kaunti ya Nyandarua, Bi Mary Wanjiru aliraukia kibanda chake cha kuuzia viazi kama kawaida.

Alisema kuwa hali ngumu ya maisha ndiyo ilimlazimu kuamka ili kuhakikisha watoto wake wamepata chakula na karo ya shule.

Alisema kwamba bwanake, Bw Wycliffe Wanjohi, pia aliamkia kazi yake ya bodaboda kama kawaida.

“Sisi huwa tunaonyeshana mapenzi kila siku. Hivyo, si lazima aninunulie maua. Cha muhimu ni kuhakikisha kwamba tuna chakula cha kutosha kuwalisha watoto wetu na kukidhi mahitaji yale mengine ya nyumbani,” akasema Bi Wanjiru.

Hali ni iyo hiyo katika kituo cha kibiashara cha Gwa Kung’u, kilicho katika kaunti iyo hiyo.

Kwenye pitapita zetu, tunakutana na Bw James Gakunya, ambaye ni mkulima.

Amebeba jembe, akielekea shambani mwake, lililo katika eneo la Equator.

Huu ni wakati ambapo watu wanatayarisha mashamba yao kwa msimu wa upanzi, kuanzia Machi.

Kulingana naye, Valentino ni “tamaduni ya Wazungu iliyowaharibu Waafrika wanaozingatia na kuiga tamaduni za kigeni”.

Anasema kuwa haitambui hata kidogo, kwani yeye huwa anaonyesha mapenzi ya dhati kwa mke na watoto wake kwa kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji yao ya kimsingi bila tatizo lolote.

“Kama mwanamume, ukamilifu wangu huwa unadhihirishwa na juhudi ninazoweka katika kuhakikisha familia yangu inapata mahitaji yake bila matatizo yoyote. Kuna haja gani ninunulie mke wangu maua, ikiwa sijatimiza mahitaji yake ya msingi pamoja na watoto wetu? Pia, pesa hizo za maua ninaweza kununulia bidhaa muhimu kama unga au mchele. Siitambui siku hiyo hata kidogo,” akasema huku akielekea shambani mwake.

Katika kijiji cha Cauri, kilicho viungani mwa mji wa Mairo Inya, wakazi wengi walikuwa mashambani mwao. Hawakuwa na ufahamu wowote wa Siku ya Valentino.

Ni vijana wachache tu walioonekana kufahamu uwepo wake, japo walisema waliamua kwenda kazini kwani “hawana muda wa kusherehekea siku hiyo”.

“Hiyo huwa ni siku ya watu wanaoishi mijini. Ingawa huwa tunaisoma kwenye mitandao, watu wengi hapa mashambani hawana wakati wa kutumia pesa kwenda mijini kuwanululia wake au mabwana zao maua. Kila siku huku huwa ni kazi. Huwa tunaonyeshana mapenzi kila siku,”asema barobaro Ken Kariuki, 27, ambaye ana watoto wawili.