‘Sababu zangu kuoa manyanga’

‘Sababu zangu kuoa manyanga’

Na LEONARD ONYANGO

KATIBU wa Muungano wa Wafanyakazi nchini (Cotu) Francis Atwoli, ameeleza hadharani sababu zake za kuoa mke wa pili; tena mbichi kabisa kiumri.

Bw Atwoli alisema Jumapili kuwa hatua yake ya kuoa mke wa pili, ambaye ni mtangazaji habari Mary Kilobi, haikutokana na uchu, bali hitaji la kuwa na mtu anayeweza kumsaidia kimaisha anapoendeleza pilkapilka zake nyingi nchini na kimataifa.

Katibu huyo mkuu wa Cotu aliyekuwa akizungumza katika Kaunti ya Kakamega alikoongoza hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Kanisa la Seventh-Day Adventist, Ebukwala, Khwisero, alisema kuwa wadhifa wake katika muungano wa Cotu humhitaji kusafiri sana ndiposa akahitaji mwanamke wa kumtunza.

“Kwa mfano, sasa niko hapa, baadaye nitaabiri ndege kwenda Nairobi ambapo nitapanda ndege kubwa kuelekea Brussels, Ubelgiji. Nitakaporudi, nitaenda Mombasa kuadhimisha Sherehe za Mashujaa na kisha kufunga safari kuelekea Uswisi, China na India. Nimeanza kuwa mzee. Ninataka dawa, ninataka mtu anayeweza kukumbuka kuniambia kwamba saa yako ya mkutano fulani imefika,” akaeleza umati.

Aliongeza, “Mnajua sasa mama watoto wangu (mke wake wa kwanza) ni ‘meneja’ wa boma hapa nyumbani. Nikisema kwamba nianze kutoka naye kila saa nitajipata sina boma. Nahitaji mke wa kunitunza hasa ninapokuwa safarini na mke mwingine wa kusimamia boma langu.”

Katibu huyo wa Cotu alisema wadhifa wake wa ukatibu unamfanya kusafiri sana, hivyo basi alihitaji mwanamke wa kumtunza.

Kulingana naye, haya yote yanamwezesha kufanikisha jukumu la kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini.

“Watu wengine wanaooa huwa ni kwa tamaa lakini mimi si kwa ajili ya tamaa. Mimi nilioa mke wa pili kwa ajili ya kazi ambayo hawa walinipa,” akasema.

Mmoja tu

Kinaya ni kwamba, aliwataka vijana kuzingatia maandiko ya Biblia na kuoa mwanamke mmoja tu.

Wakati huo huo, Bw Atwoli alipuuzilia mbali wito wa Naibu Rais William Ruto kutaka kuunganisha Waluhya huku akisema kuwa jamii hiyo haihitaji msaada kutoka nje.

Bw Atwoli alisema kuwa jamii ya Waluhya imeungana ‘lakini kuna viongozi wachache ambao wamekuwa wakiyumbayumba kisiasa kwa maslahi yao ya kibinafsi’.

“Jamii ya Waluhya haijagawanyika, kuna wachache tu ambao wanatembeza matumbo yao kwa maslahi yao ya kibinafsi,” akasema.

Wiki iliyopita, Dkt Ruto alijitolea kusaidia kuwaunganisha kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula ili kuhakikisha kuwa wanazungumza kwa sauti moja na hata kuunga mkono mwaniaji wa Jubilee McDonald Mariga katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika eneobunge la Kibra utakaofanyika Novemba 7.

You can share this post!

UDAKU: Nioe nikujazie dunia, kichuna amlilia Ronaldo

Moi afanyiwa uchunguzi wa kiafya jijini Nairobi

adminleo