Michezo

Sababu zitakazowavunia Barcelona au City ufalme UEFA

April 15th, 2019 2 min read

NA MWANDISHI WETU

MECHI za maruadiano ya robo-fainali za kuwania taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu zitasakatwa wiki hii huku Barcelona na Juventus zikitarajiwa kuwa timu za kwanza kutinga hatua ya nusu-fainali.

Miamba wa soka ya Uingereza, Manchester City watachuana na Tottenham Hotspur uwanjani Etihad mnamo Jumatano, siku ambapo Liverpool nao wanatazamiwa kutua nchini Ureno kurudiana na FC Porto.

Barcelona watakuwa kesho wenyeji wa Manchester United ugani Camp Nou huku Juventus wakialika Ajax ya Uholanzi jijini Turin, Italia.

Chini ya mkufunzi Ernesto Valverde, Barcelona watashuka dimbani wakitawaliwa na hamasa ya kusajili ushindi muhimu wa 1-0 uwanjani Old Trafford katika mchuano wa mkondo wa kwanza wiki jana. Kikosi hicho pia kinapigiwa upatu wa kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na Copa del Rey.

Japo kocha Ole Gunnar Solskjaer ana wingi wa imani kwamba vijana wake watatamba ugenini kama walivyofanya dhidi ya PSG katika hatua ya 16-bora, kibarua kichopo mbele yao ni kigumu na kizito zaidi.

Barcelona wanatazamiwa kulipiza kisasi kwa kukizamisha chombo cha Man-United kirahisi na kujikatia tiketi ya kuchuana na Liverpool kwenye hatua ya nne-bora.

Man-United wanajivunia kushinda Barcelona mara moja pekee katika jumla ya mechi nane zilizopita. Walitawazwa mabingwa wa UEFA mara ya mwisho mnamo 2008 baada ya kuwalaza Chelsea nchini Urusi. Mwaka huo, Man-United waliwabandua Barcelona? ambao ni mabingwa mara tano wa UEFA katika hatua ya nusu-fainali.

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp watajibwaga uwanjani Estadio do Dragao mnamo Jumatano wakijivunia ushindi wa 2-0 waliousajili dhidi ya Porto ugani Anfield mapema wiki jana.

Liverpool ambao pia ni mabingwa mara tano wa UEFA, hawajapoteza dhidi ya Porto katika jumla ya mechi saba zilizopita.

Baada ya kuwadengua Porto, basi mtihani mgumu zaidi uliopo mbele ya Liverpool ni kuwakung’uta Barcelona ambao iwapo wataponea, basi watajiweka pazuri zaidi kunyanyua ubingwa wa UEFA msimu huu kwa kuwapiku ama Man-City au Juventus.

Historia inawaweka Barcelona katika nafasi nzuri zaidi ya kuwapepeta Liverpool na hivyo kutinga fainali ambayo kwa asilimia kubwa, inatazamiwa kuwakutanisha na Man-City wanaofukuzia mataji manne chini ya kocha Pep Guardiola.

Kikosi hicho kinatarajiwa kuwika zaidi mbele ya mashabiki wa nyumbani na kubatilisha matokeo ya 1-0 yaliyosajiliwa na Tottenham dhidi yao wiki jana.

Ushindi kwa Man-City utawapa hamasa zaidi ya kuwakomoa Juventus katika nusu-fainali. Chini ya mkufunzi Massimiliano Allegri, Juventus wanaojivunia huduma za Cristiano Ronaldo, wanatazamiwa kuwazima Ajax waliowalazimishia sare ya 1-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza.

Ajax ambao ni wafalme mara nne wa UEFA, hawana ushindi katika mechi nne zilizopita dhidi ya Juventus walionyanyua mabingwa mnamo 1985 na 1996.

Chelsea iliyopiga Bayern Munich 4-3 kupitia penalti mnamo 2011-12, ndiyo klabu ya mwisho inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuwahi kutia kapuni ufalme wa UEFA.