Habari Mseto

Sabina alia tena katika ziara ya Embrace Nyanza

June 28th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

MWAKILISHI wa Wanawake katika Kaunti ya Murang’a Sabina Chege, alibubujikwa na machozi Ijumaa aliposikia masaibu ambayo wakazi wa Kaunti ya Kisumu walipitia kwenye ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa 2017.

Bi Chege na viongozi wengine 30 wanawake wanachama wa kundi la Embrace walitekwa na hisia wakiwa nyumbani kwa wazazi wa mtoto Pendo aliyeuawa wakati wa ghasia za uchaguzi uliopita.

Viongozi hao waliahidi kushinikiza jamaa za waliouawa, kujeruhiwa au kupoteza mali yao walipwe fidia. Waliwaahidi wakazi kwamba matatizo yao yatasuluhishwa mwaka huu wa matumizi ya pesa za serikali.

“Tunawaahidi kwamba tutawasilisha mswada wa fidia katika Bunge la Kitaifa wiki ijayo ili suala hilo liweze kutatuliwa mara moja,” alisema.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Homa Bay, Bi Gladys Wanga alisema wataweka mikakati ya kisheria itakayoisaidia serikali kuwalipa fidia watu wote ambao waliteseka kwa namna yoyote kwenye ghasia hizo.

“Vilevile, tutahakikisha kuwa hatua kali zimechukuliwa dhidi ya wale ambao wametajwa kuchochea au kushiriki katika ghasia hizo,” alisema baada ya kuwatembelea wazazi wa Mtoto Pendo, ambaye aliuawa na polisi kwenye ghasia zilizotokea katika mtaa wa Nyalenda mnamo 2017.

“Hakuna mwanamke ambaye anapaswa kumpoteza mwanawe tena kutokana na uchaguzi. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa hakuna ghasia zinazotokea na kuzua chuki za kisiasa na kikabila,” akasema mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko.

Viongozi hao baadaye walihutubia mkutano katika uwanja wa michezo wa Jomo Kenyatta, ambapo waliunga mkono handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.