Habari

Sabina Chege alaumiwa kwa 'kutega bomu' la mihadarati nchini

May 31st, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

BAADHI ya viongozi wa kidini, wadau katika vita dhidi ya mihadarati na viongozi wamepinga kwa kauli moja pendekezo linaloonekana kulegeza msimamo kuhusu watumiaji wa dawa za kulevya kwa kutaka sheria na kanuni mbalimbali kuwatambua kama wagonjwa na wala sio wavunjaji sheria.

Walisema Alhamisi kufanya hivyo ni sawa na kuhalalisha mihadarati hapa nchini.

Wote walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kujitokeza mara moja na kusema kuwa hiyo si sera ya serikali yake na kamwe hatawahi kukubalia rasilimali za taifa zitumiwe kuandaa harakati za kupitisha sheria hizo.

Kasisi Peter Mburu aliye mwenyekiti wa makanisa asili nchini alisema kuwa ikiwa kutaandaliwa vikao vya umma kusaka maoni kuhusu pendekezo hilo, washirikishi watimuliwe na ikiwezekana, wakamatwe kwa kujaribu kupigia debe uovu wa kijamii.

Waliungana kusuta vikali kamati ya bunge kuhusu afya ambayo ilifichua njama ya kuunda sheria bungeni ya kutoadhibu wote watakaonaswa wakitumia mihadarati nchini kwa msingi wa kuwasaidia kuwarekebisha tabia na mienendo.

Mwenyekiti wea kamati hiyo Bi Sabina Chege alitetea sera hiyo akiitaja kama iliyojaribiwa na kufaulu katika taifa la Ureno na ikafaulu kuzima vijana wengi waliokuwa wamezama katika uraibu wa matumizi ya mihadarati kurekebishwa mienendo.

Bi Chege alisema kuwa watumizi wa mihadarati huwa ni wagonjwa bali sio wavunjaji sheria wanaofaa kuadhibiwa kwa ama vifungo gerezani au faini mahakamani.

Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Kadinali John Njue alitaja pendekezo hilo kuwa mzaha mkuu na ambao nia ya kipekee inaweza kuwa tu kugeuza jumuiya ya vijana wa taifa hili kuwa iliyokalia bomu la kutegwa.

“Huwezi ukasema kuwa ni uongozi unaomakinika kuwazia kuleta sera ya kuhalalisha mihadarati nchini. Ni sawa na kusema ukinasa wabakaji wasiandamwe kisheria bali wasaidiwe kurekebisha mienendo. Hakuna uhalali wowote katika mjadala huu na tutaupinga kwa dhati,” akaambia Taifa Leo.

Mwenzake wa Kanisa la Kipresibeteria Julius Guantai alisema kuwa kusema vijana waingizwe katika uhalali wa utumizi wa mihadarati hata kwa asilimia 0.01 ni sawa na kuchukua njia ya mkato kufika jehanamu.

Waliokuwa wenyekiti wa mamlaka ya kupambana na mihadarati nchini (Nacada) Mbw Joseph Kaguthi na John Mututho waliungama kuwa wazo hilo lina ulemavu wa kimaadili.

Umoja wa dini ya Kiislamu nchini (Supkem) kupitia mwenyekiti wake Prof Abdulghafur El-Busaidy alisema sera kama hiyo ni ya kuangamiza taifa na vijana kwa ujumla na kuzima kesho ya taifa hili.

“Utawezaje kuwazia kuhalalisha mihadarati nchini? Unasema eti utaweka mikakati ya kufahamu wale walio katika uraibu huo kama watumizi na

walio katika uraibu huo kama wafanyabviashara wa ulanguzi. Ikiwa unajali taifa hili na janga la mihadarati, mbona usiweke sheria za kuzima uingizaji na kilimo cha mihadarati hapa nchini?” akasema.

Prof Busaidy alisema kuwa sera kama hiyo inaweza tu kuwa na lengo moja la kusaidia mabwanyenye walio ndani ya biashara ya mihadarati nchini mwanya wa kibiashara.

“Hii ni sera ya kuwapa kinga walanguzi bali sio ya kusaidia jamii kwa lolote,” akasema.

Mkurugenzi wa Shirika la kupambana na utumizi wa mihadarati barani Afrika (Masaa) Bw Richard Gakunju alisema kuwa yeye ni daktari na hajapata umakinifu wowote katika tetesi za Bi Chege.

“Wale vijana wanaoanza kutumia mihadarati hawatakuwa na ule uzoeefu wa kutumia kiwango kikubwa. Sasa hao tuseme ni wagonjwa ilhali hata hajatumia mihadarati kwa siku mbili? Wale wajanja katika biashara hii si watawahamasisha wateja wao kuwa bora wapatikane tu na kiwango kidogo cha mihadarati hawatasakamwa na sheria? Wakati sheria zimewekwa za kudhibiti utoaji au uwekaji wa vitita vikubwa vya pesa katika benki za Kenya, si wajanja huweka pesa zao nyumbani?” akahoji.