Saburi akubali kuunga mkono Mung’aro kwa ugavana Kilifi

Saburi akubali kuunga mkono Mung’aro kwa ugavana Kilifi

NA WINNIE ATIENO

ALIYEKUWA waziri msaidizi wa ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, amepata afueni baada ya mpinzani wake, Bw Gideon Saburi kukubali kumuunga mkono kwa ugavana Kilifi.

Bw Saburi alikuwa akimezea mate tikiti ya ODM kuwania urithi wa kiti cha Gavana Amason Kingi, na baada ya tikiti kumwendea Bw Mung’aro, alikuwa miongoni mwa waliotarajiwa kuchaguliwa kuwa mgombea mwenza.

Alisema uamuzi wake kukubali kumuunga mkono mwenzake, ulitokana na mikutano aliyofanya na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, na naibu kiongozi wa chama, Bw Hassan Joho aliye pia gavana wa Mombasa.

Bw Mung’aro alimchagua Bi Flora Chebule, ambaye ni mwanawe mbunge wa zamani wa Kaloleni Dkt Chibule wa Tsuma, kuwa mgombea mwenza wake.

“Ninafurahi sana kuteuliwa kwa Bi Chebule ambaye ni mtaalamu wa elimu. Nilishawishiwa na Bw Odinga na Bw Joho kujiondoa na kuahidiwa nafasi ya kutumikia umma katika serikali ya kitaifa. Nitahakikisha wakazi wa Kilifi wananufaishwa na serikali ya kitaifa,” alisema Bw Saburi.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi, Bw Jimmy Kahindi, ambaye pia alikuwa akiwania tikiti hiyo, aliamua kuhamia Chama cha UDA.

Bw Saburi aliwasihi wakazi wa Kilifi kumuunga mkono Bw Odinga ili kaunti hiyo inufaike na serikali ya kitaifa.

Bw Mung’aro alimshukuru Bw Saburi kwa kumuunga mkono akaahidi kufanikisha mipango ya kuimarisha viwanda, kufufua ajira, kuwekeza kwenye sekta ya kilimo, maji na elimu.

Wakati uo huo viongozi wa ODM Kilifi walisema vuta nikuvute kati ya Gavana Kingi na Mbunge wa Malindi Bi Aisha Jumwa ambaye anagombania ugavana ni afueni kwa Bw Mung’aro.

Wabunge Ken Chonga (Kilifi Kusini), Teddy Mwambire (Ganze), mwakilishi wa wanawake Bi Gertrude Mbeyu na seneta Stewart Madzayo, waliwasihi wakazi kupiga kura kwa wagombea wote wa ODM ili kuupa nguvu muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Walimpa changamoto Gavana Amason Kingi kuwaelezea wakazi namna alivyotumia fedha miaka 10 ya ugatuzi ilhali kaunti hiyo ikiendelea kukabiliana na baa la njaa na ukosefu wa maji.

Bw Chonga alisema Kilifi inafaa kukombolewa kutoka kwa uongozi mbaya.

Kwa upande wake, Bw Mwambire ambaye ni mwenyekiti wa chama cha ODM tawi la Kilifi aliwasihi wakazi kumuunga mkono Bw Odinga.

Seneta Madzayo aliapa kuhakikisha fedha za umma zinatumika vizuri.

  • Tags

You can share this post!

ODM motoni kuacha Maitha katika mataa

Jumwa sasa amrukia Ruto mvutano na Kingi ukizidi

T L