Saburi kusalia ODM wenzake wakihepa

Saburi kusalia ODM wenzake wakihepa

Na WAANDISHI WETU

NAIBU Gavana wa Kaunti ya Kilifi, Bw Gideon Saburi ametangaza atabaki katika Chama cha ODM anapopanga kuwania ugavana mwaka ujao, wakati ambapo wanasiasa wengine wengi kaunti hiyo wanahama chama hicho.

Akizungumza na wanahabari eneo la Watamu, Bw Saburi alifafanua kwamba hapingi uundaji wa chama cha Pwani lakini anaamini atafanikiwa kujikuza zaidi kisiasa akiwa ndani ya ODM.

“Ninataka kuweka wazi kwamba sitajihusisha na siasa za mirengo bali nitaendelea kukitumikia chama cha ODM. Chama hicho ndicho kiliniwezesha kufika hapa nilipo,” akasema Bw Saburi.

Bw Saburi ni miongoni mwa wanasiasa wa kaunti hiyo ambao wanajinoa makali kung’ang’ania urithi wa kiti cha Gavana Amason Kingi ambaye atakamilisha kipindi chake cha pili cha uongozi mwaka ujao.

Wanasiasa wengine wanaomezea mate kiti hicho ambao ni wanachama wa ODM tayari walitangaza mipango ya kuhamia vyama tofauti.

Baadhi yao ni Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa ambaye ameegemea Chama cha United Democratic Alliance (UDA), na Mbunge wa Magarini Michael Kingi ambaye alisema anasubiri chama cha Pwani kitakachoundwa.

Hata hivyo Saburi alidai kuwa yeye ndiye anastahili zaidi kurithi kiti cha Gavana Kingi, ambaye anaongoza juhudi za kuunda chama cha Pwani licha ya kuwa yeye ni mwenyekiti wa ODM Kilifi.

“Kwa kuwa nina uzoefu wa uongozi wa kaunti, bila shaka Kilifi itaimarika zaidi na ifikapo 2022 mimi nitakuwa kwenye debe,’ akasema.

Kwingineko katika Kaunti ya Mombasa, mfanyabiashara Suleiman Shahbal alijiuzulu rasmi kutoka Chama cha Jubilee anapojiandaa kuwania kiti kinachoshikiliwa na Gavana Hassan Joho mwaka ujao.

Bw Shahbal ambaye wiki chache zilizopita alikuwa ametangaza nia ya kujiunga na ODM, aliandika barua kwa Jubilee kuomba kuondoka chamani.

“Ningependa kuchukua nafasi hii kushukuru Chama cha Jubilee kwa usaidizi wote ambao kilinipa wakati nilipokuwa mwanachama,” akasema katika barua ambayo ilitumwa pia kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Hii itakuwa mara yake ya tatu kuwania ugavana kupitia chama tofauti, baada ya kujaribu alipokuwa mwanachama wa Wiper 2013 na Jubilee 2017. Atashindania tikiti ya ODM na Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir.

Wakati huo huo, baadhi ya wazee wa jamii ya Mijikenda wamempendekeza Bw Samuel Mwaro kuwa mwaniaji ugavana ambaye anastahili kuungwa mkono na jamii hiyo Mombasa.

Bw Mwaro hufahamika kwa kusimamia mashirika yanayotoa huduma muhimu za kijamii.Wazee hao wakiongozwa na Bw Shafi Makazi walimkabidhi Bw Mwaro kiti kidogo kilichoundwa kwa mbao, kuashiria wamemtawaza kuwania uongozi kwa niaba ya jamii.

You can share this post!

Jamii ndogo zataka Rais abuni wizara iwasaidie

Simulizi ya mama yashtua mahakama