Habari Mseto

'Saburi sasa aweza kushtakiwa baada ya kupona corona'

April 2nd, 2020 1 min read

JUMA NAMLOLA na MAUREEN ONGALA

NAIBU gavana wa Kilifi, Bw Gideon Saburi sasa anakodolea macho kushtakiwa, baada ya vipimo kuonyesha kuwa amepona kutokana na corona.

Alhamisi, waziri wa Afya Bw Mutahi Kagwe alisema Bw Saburi ambaye wiki hii aliomba radhi kwa kutangatanga eneo la Pwani baada ya kutoka Ujerumani, amepona kabisa.

“Naibu gavana wa Kilifi sasa hana tena corona. Tunaachia vyombo vya sheria vishughulike naye,” akasema.

Bw Saburi alizua wasiwasi eneo zima la Pwani, aliporejea kutoka Ujerumani Machi 9 na kukosa kujifungia nyumbani. Alitangamana na watu katika maeneo mbalimbali ya Kilifi, Mombasa na Kwale, kabla ya kugunduliwa kuwa alikuwa ameambukizwa, alipopimwa Machi 20.

Alikataa matokeo hayo na kudai ilikuwa njama ya kumharibia jina. Serikali ililazimika kumchukua kwa nguvu na kumpeleka katika hospitali ya Mbagathi, Nairobi.

Kitendo chake kilimkera hata Rais Uhuru Kenyatta, ambaye kwenye mojawapo ya hotuba zake alimkemea na kusema alionyesha mfano mbaya.

Mbali na kutangamana na viongozi wakuu wa Kilifi, Bw Saburi yasemekana alihudhuria mazishi katika sehemu tatu tofauti na harusi eneobunge la Rabai.

Mbali na mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Msambweni, Bw Suleiman Dori, naibu huyo wa gavana alitangamana na watu wengi mjini Mtwapa. Miongoni mwa watu waliopelekwa karantini baada ya tukio hilo, ni maafisa 17 wa polisi wa kituo cha Mtwapa.

Mbunge wa Rabai Bw William Kamoti na gavana Amason Kingi pia walienda karantini baada ya tukio hilo.

Iwapo atapatikana na hatia, huenda Bw Saburi akavuliwa mamlaka yake.