HabariSiasa

Saburi akamatwa baada ya kupona corona

April 3rd, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

NAIBU Gavana wa Kilifi, Gideon Saburi, alikamatwa Ijumaa na maafisa wa DCI katika hospitali kuu ya Pwani, siku moja tu baada ya kupona maradhi ya Covid-19.

Maafisa zaidi ya wanane, wakiongozwa na mkuu wa DCI eneo hilo, Bw Washington Njiru, waliwasili katika hospitali hiyo nyakati za mchana na kumtia pingu Bw Saburi. Walimwingiza kwenye gari na kuondoka naye.

Bw Saburi alipelekwa katika kituo cha polisi cha Urban, ambapo kufikia wakati wa kutayarisha ripoti hii, alikuwa anaandikisha taarifa yake kwa polisi.

Naibu huyo wa gavana alikamatwa siku moja baada ya Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe kusema anastahili kunyakwa kwa kutojitenga aliporejea nchini kutoka Ujerumani.

Bw Saburi alionekana kuwa amepata virusi hivyo, baada ya kuchukuliwa kwa lazima na kutengwa.

Serikali inasema alidinda kujitenga tangu Machi 7 ambapo aliwasili nchini. Iliripotiwa kuwa aliamua kuhudhuria mazishi katika maeneo mbalimbali ya Pwani, yakiwemo ya aliyekuwa Mbunge wa Msambweni, Suleiman Dori na mengine eneobunge la Rabai ambapo alitangamana na viongozi kadhaa waliolazimika kujitenga na watu.

Mmoja wa viongozi hao baadaye alipatikana kuwa ameambukizwa virusi hivyo.? Gavana Amason Kingi alikuwa amemueleza Bw Saburi achukue mapumziko ya siku 30 lakini akakiuka agizo hilo. Badala yake, aliamua kuendelea kuchapa kazi.

Ripoti zilionyesha kuwa, mnamo Machi 16, Bw Saburi alifika afisini mwake na akafanya mikutano kadhaa na wafanyakazi wake. Baadaye, mmoja wa wafanyakazi wa kaunti ya Kilifi alihimiza Bw Saburi atafutwe na ndipo akapatikana akiwa eneo la Mtwapa.

Akiwa huko, yasemekana alikuwa akitangamana na watu wengine, wakiwemo maafisa wa polisi wa kituo cha Mtwapa.

Baadhi ya maafisa hao baadaye walitengwa, mmoja alipoonyesha dalili za kupata matatizo ya kupumua.? Siku sita baada ya kuchukuliwa kwa nguvu na kutengwa, Bw Saburi aliomba msamaha kwa Wakenya kwa yote aliyotenda.

“Najua nimeleta uchungu kwa kueneza virusi hivi eneo la Kilifi na nchini mwetu kwa jumla. Naomba munisamehe,” akasema Bw Saburi.? Vilevile, mhandisi huyo ambaye ni baba wa watoto watatu, aliwahimiza Wakenya kuwa makini na kufuata amri za serikali na maelezo mengine yoyote kuhusiana na ugonjwa huu wa Covid-19.