Sadio Mane aendea mamilioni ya Bayern Munich

Sadio Mane aendea mamilioni ya Bayern Munich

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp ametaka mashabiki kutarajia makuu zaidi kutoka kwa Liverpool msimu ujao licha ya miamba hao kuagana na fowadi matata raia wa Senegal, Sadio Mane.

Mane atakayevalia jezi za Bayern Munich ya Ujerumani kwa mihula mitatu ijayo akilipwa Sh53 milioni kwa wiki, anabanduka ugani Anfield baada ya miaka sita iliyomshuhudia akifungia Liverpool mabao 120 kutokana na mechi 269.

Pengo lake uwanjani Anfield tayari limezibwa na mshambuliaji mahiri raia wa Uruguay, Darwin Nunez, atakayeshirikiana na Mohamed Salah, Luis Diaz, Roberto Firmino na Diogo Jota katika safu ya mbele ya Liverpool.

Nunez, 22, alisajiliwa na Liverpool kutoka Benfica ya Ureno kwa ada ya awali ya Sh9.5 bilioni itakayoongezeka baadaye hadi Sh12.6 bilioni. Alifungia Benfica mabao 34 kutokana na michuano 41 katika mashindano yote mnamo 2021/22. Magoli 26 kati ya hayo yalitokana na mechi 28 za Ligi Kuu ya Ureno.

“Nunez alimpisha Mane ambaye amekuwa kati ya wanasoka wetu tegemeo. Muhimu zaidi ni kusalia imara na thabiti licha ya mabadiliko hayo. Pia tumemsajili Fabio Carvalho kutoka Fulham. Tunalenga kunyanyua mataji mawili yaliyotuponyoka – Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA),” akasema Klopp.

Mane aliyekuwa akidumishwa na Liverpool kwa Sh14.8 milioni kwa wiki, anatazamiwa kuingia katika sajili rasmi ya Bayern wiki ijayo kwa Sh6 bilioni ili kujaza nafasi ya kigogo Robert Lewandowski anayewaniwa na Barcelona, Chelsea, Man-United na Paris St-Germain (PSG).

Liverpool watapokea kwanza Sh4 bilioni kutoka kwa Bayern na nyongeza ya Sh1 bilioni kutegemea idadi ya mechi zitakazopigwa na Mane na Sh1 bilioni zaidi kutegemea mafanikio yatakayoletwa na sogora huyo wa zamani wa Southampton ugani Allianz Arena.

Mane, 30, ndiye mchezaji wa kwanza wa haiba kubwa kusajiliwa na Klopp kambini mwa Liverpool. Nyota huyo aliyeongoza Senegal kuzamisha Misri na kutwaa Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Februari mwaka huu nchini Cameroon, aliagana na Southampton kwa Sh4.9 bilioni mnamo 2016.

Tangu wakati huo, amefungia Liverpool mabao 90 katika EPL huku akicheka na nyavu za wapinzani mara 23 kutokana na mashindano yote ya msimu wa 2021-22 ulioshuhudia waajiri wake wakizoa Kombe la FA na Carabao Cup.

Mane, Salah na Firmino waliwezesha Liverpool kutawazwa wafalme wa UEFA mnamo 2019 kabla ya kunyanyulia kikosi hicho taji la kwanza la EPL baada ya miaka 30 mnamo 2020.

Ushirikiano wao uliokuwa mwiba mkali kwa wapinzani wao katika EPL na soka ya bara Ulaya, ulizalisha mabao 338 katika kipindi cha misimu mitano kwenye mashindano yote.

Mbali na Mane, wavamizi wengine wanaotazamiwa kubanduka Liverpool ni Takumi Minamino na Divock Origi anayehusishwa pakubwa na AC Milan ya Italia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza wawataka maseneta...

Akinyi na Kangangi wachupa uongozoni mbio za baiskeli za...

T L