Sadio Mane aongoza Bayern kubomoa Frankfurt katika Bundesliga

Sadio Mane aongoza Bayern kubomoa Frankfurt katika Bundesliga

Na MASHIRIKA

SADIO Mane alifunga bao katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) na kusaidia Bayern Munich kuanza kampeni za ligi muhula huu kwa ushindi mnono wa 6-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt mnamo Ijumaa usiku ugani Deutsche Bank Park.

Nyota huyo raia wa Senegal alijaza kimiani bao la tatu la Bayern waliojivunia uongozi wa magoli 5-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza. Wanasoka wengine waliofunga mabao ya Bayern ni Joshua Kimmich, Benjamin Pavard, Serge Gnabry na Jamal Musiala.

Frankfurt waliofutiwa machozi na Randal Kolo Muani, walishinda Europa League msimu jana na watavaana na wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Real Madrid, katika gozi la Uefa Super Cup mnamo Jumatano ijayo.

Mane alijiunga na Bayern mnamo Juni baada ya kuondoka Liverpool kwa Sh5 bilioni. Sogora huyo atakayevalia jezi za Bayern kwa misimu mitatu ijayo akilipwa Sh53 milioni kwa wiki, alibanduka ugani Anfield baada ya miaka sita iliyomshuhudia akifungia Liverpool mabao 120 kutokana na mechi 269.

Alifungua akaunti yake ya mabao kambini mwa Bayern wiki moja iliyopita baada ya kuongoza waajiri wake kukomoa RB Leipzig 5-3 na kutwaa taji la German Super Cup ugani Red Bull Arena.

Kusajiliwa kwake kulichochewa na haja ya kujaza pengo la kigogo Robert Lewandowski aliyeyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona. Mane aliongoza Senegal kutandika Misri kwa penalti 4-2 na kutwaa Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Februari mwaka huu nchini Cameroon.

Aliagana na Southampton kwa Sh4.9 bilioni mnamo 2016 na kutua Liverpool aliowafungia mabao 90 huku 23 yakitokana na kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2021-22.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Zelensky ashutumu shirika la Amnesty kwa kutuhumu wanajeshi...

TAHARIRI: Twapongeza wanariadha wetu kuletea Kenya fahari

T L