Michezo

SAFARI RALLY: Barabara za Kenya zahitaji ujasiri, wasema madereva wa kimataifa

September 15th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MADEREVA wa kimataifa wanasubiri kwa hamu kubwa kushiriki mbio za magari za Safari Rally zitakazorejea kwenye ratiba ya Shirikisho la Mbio za Magari Duniani (WRC) mwaka 2021.

Wakizungumza na tovuti ya www.wrc.com, madereva shupavu walitaja barabara za Kenya zinazohitaji ujasiri mkubwa pamoja na wanyama pori kuwa vitu vinavyowapa hamu zaidi ya kuja Kenya kwa duru hiyo iliyofanyika mara ya mwisho kwenye WRC mwaka 2002.

Duru ya Safari Rally ilikuwa imeratibiwa kurejea kwenye kalenda hiyo mwaka 2020, lakini ikasukumwa hadi 2021 kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona ambavyo vimesababisha maafa kote duniani.

WRC imethibitisha kuweka Safari Rally kwenye ratiba ya kwanza ya 2021 ili kujulisha madereva duru zitakazoshindaniwa msimu ujao.

Bingwa mara tisa wa dunia Sebastian Loeb alishiriki Safari Rally mwaka 2002 kabla duru hiyo kuondolewa kutokana na ukosefu wa fedha. Mwaka huo, Loeb alikamilisha Safari Rally katika nafasi ya tano nyuma ya Muingereza Colin McRae, Mfini Harri Ravanpera, Mswidi Thomas Radstrom na raia wa Estonia Markko Martin walionyakua nafasi nne za kwanza, mtawalia.

“Nina kumbukumbu nzuri za Safari Rally pale tuliona tumbili na twiga kwenye mbuga za wanyama zilizotumiwa kwa mashindano ambayo pia yalishuhudia helikopta zikipaa juu ya kila gari kufukuza wanyama barabarani. Yalikuwa mashindano yasiyo na kifani,” Mfaransa Loeb,46, aliambia tovuti hiyo.

Bingwa mara sita wa dunia Sabastien Ogier huenda akalazimika kuchelewesha mipango yake ya kustaafu mwaka 2020 ili ashiriki Safari Rally mwaka ujao. Mfaransa Ogier alisema, “Tukirejelea historia, mbio za Safari Rally zilikuwa za kipekee kwenye kalenda. Hata leo, sidhani kama zimebadilika sana. Natarajia ziwe na msisimko na ngumu.”

Ogier,36, ambaye yuko katika timu ya magari ya Toyota Gazoo Racing, alifagia mataji ya dunia ya mwaka 2013, 2014, 2015, 2016, 2017 na 2018. Akiwa ameshinda duru 48 na kujivunia mataji sita ya dunia, Ogier ndiye dereva wa pili aliyepata ufanisi mkubwa kwenye mbio za WRC baada ya Loeb waliyewahi kushirikiana naye katika timu moja ya Citroen.

Tommi Makinen,56, ambaye ni mmoja wa madereva wa WRC waliong’ara miaka ya ‘90, anakumbuka Safari Rally kwa hamu kubwa. Raia huyo wa Finland, ambaye aliibuka bingwa wa dunia mwaka 1996, 1997, 1998 na 1999 akipeleka gari la aina ya Ralliart Mitsubishi Lancer Evolution, anasema mbio za Safari Rally zilikuwa kipimo cha uvumilivu na wala sio tu kushindania alama.

“Ni duru ambayo ingekupatia kila kitu, kutoka kwa wanyama hadi barabara zinazohitaji umakinifu na ujasiri mkubwa,” alisema bingwa huyo wa Safari Rally mwaka 1996 na 2001, ambaye sasa ni kiongozi wa timu ya Toyota Gazoo Racing.

Bingwa wa dunia mwaka 2019 Ott Tanak kutoka Estonia, ambaye anapeperusha bendera ya timu ya Hyundai, pia alisifu Safari Rally. Dereva huyo mwenye umri wa miaka 32 alisema, “Safari ni kitu tofauti sana na spesheli. Kupata fursa ya kuona twiga na ndovu kutaongeza msisimko katika duru hiyo mwaka ujao na pia barabara zitakazotumika.”

Tanak alikamilisha msimu wa 2017 na 2018 katika nafasi ya pili nyuma ya Thierry Neuville na Ogier, mtawalia. Kisha, alinyakua taji lake la kwanza la dunia mwaka 2019.

Ufanisi wake ulimuingiza katika mabuku ya historia kwa kuwa dereva wa kwanza kutoka Estonia kuwa bingwa wa dunia, wa kwanza asiye Mfaransa tangu raia wa Norway Petter Solberg mwaka 2003 na kushindia Toyota taji la dunia kwa mara ya kwanza tangu Didier Auriol atawale mwaka 1994.

Wakati huo huo, Kenya inajitahidi kuhakikisha Safari Rally 2021 inakuwa sawa kabisa. Afisa Mkuu Mtendaji wa Safari Rally Phineas Kimathi ameshukuru serikali kwa mchango wake mkubwa ambao umehakikisha mipango ya duru hiyo iko kabambe.

“Nashukuru serikali kwa kujitolea  na pia namshukuru Waziri wa Michezo Amina Mohamed kwa uongozi na ushauri kuhakikisha tunapokea usaidizi unaohitajika,” alisema mwenyekiti huyo wa Shirikisho la Mbio za Magari nchini Kenya (KMSF).

Baadhi ya madereva matata Kenya inajivunia ni Baldev Chager, ambaye aliibuka mshindi wa msimu uliopita nchini Kenya, Carl ‘Flash’ Tundo na bingwa wa Bara Afrika Manvir Baryan.