Makala

Safari ya Lamu-Garsen ilivyo ziara ya mbugani kujionea wanyamapori

May 29th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

MSAFIRI kwenye barabara kuu ya Lamu-Garsen mara nyingi hulinganishwa na mtalii anayefanya ziara kwenye mbuga mashuhuri nchini.

Hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wanyamapori wapatikanao kwenye misitu ya kandokando mwa barabara hiyo ambayo ndio kiunganishi cha pekee kati ya Lamu na sehemu nyingine za nchi kupitia nchi kavu.

Unaposafiri kwenye barabara ya Lamu-Garsen na unapopita sehemu kama vile Ndeu, Milihoi, Koreni, Mkunumbi, Kibaoni, Pangani au Maisha Masha, Mambo Sasa, Witu, Lango la Simba na Nyongoro, huenda ukastaajabu kuwaona wanyama wa kila aina.

Mara nyingi msafiri huwaona wakichezacheza pembezoni mwa barabara au wakila nyasi na majani ya miti.

Twiga wakiwa Milihoi kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ni kawaida kuwaona kima, nyani, mayonda au tumbiri wakirukaruka kutoka kwa mti mmoja hadi kwa mwingine, ishara tosha huwa wanafurahia mandhari hayo sufufu yaliyokoleza rangi ya kijani kibichi, hasa kwenye eneo la Mambo Sasa.

Mahali kama vile Milihoi au Pangani sanasana utapata makundi ya twiga na punda milia wakilisha au kuvuka barabara kwa madaha, hivyo kuleta taswira kwa msafiri kwamba ni bayana eneo hilo ni mbuga tu.

Wanyama wengine waliosheheni na kuyaburudisha macho ya wapiti njia kwenye barabara ya Lamu-Garsen ni nyati, simba, paa, fisi, swara, tohe, kongoni au topi na wengineo wengi.

Bw Godana Abarufa, ambaye ni mmoja wa wasafiri wa kila mara kwenye barabara kuu ya Lamu-Garsen, aliambia Taifa Leo kuwa utajiri wa wanyamapori upatikanao Lamu wafaa kutambuliwa si Kenya tu bali ulimwenguni kote.

Bw Abarufa alisema badala ya watalii kufika Kenya na kutumia fedha nyingi kuzuru mbuga za wanyama kama vile Tsavo Mashariki, Tsavo Magharibi, Mbuga ya Kitaifa ya Wanyama ya Nairobi, Mbuga ya Kitaifa ya Maasai Mara na kwingineko, ni vyema kwao endapo watafikiria kufika Lamu kupitia barabara.

“Unaposafiri kwa gari lako au lile la usafiri wa umma (PSV) kupitia barabara yetu kuu ya Lamu-Garsen ‘utabambika’ na mamia ya wanyamapori utakaowaona. Barabara yetu iko na utajiri wa misitu inayohifadhi kila aina ya wanyama. Yaani kusafiri kwenye barabara yetu ni sawa na kutenga muda wako kuizuru mbuga ya wanyamapori,” akasema Bw Abarufa.

Kusitasita

Bi Maryam Musa, ambaye ni mkazi wa kisiwa cha Lamu, alisema haoni sababu ya kwa nini serikali inasitasita kutangaza maeneo mengi ya Lamu kuwa mbuga za wanyamapori.

Bi Musa anashikilia kuwa karibu kila aina ya wanyama pori hupatikana kwenye misitu ya Lamu kinyume na mbuga zingine nchini ambapo wanyama wengine hawapatikani.

“Serikali imetenga tu Boni-Dodori, Lamu Mashariki kuwa mbuga ya wanyama ilhali sehemu nyingi zikisalia tu vivi hivi licha ya kuwa na ukwasi wa karibu aina zote za wanyamapori. Tutafurahia tukisikia Milihoi, Pangani, Ndeu, Lango la Simba, Mambo Sasa na Nyongoro zimetangazwa kuwa mbuga ya wanyama,” akasema Bi Musa.

Naye Dan Kariuki ambaye ni mtalii wa ndani kwa ndani anayependelea sana kuzuru mbuga tofautitofauti kutazama wanyama pori aliitaja Lamu kuwa kiboko yao kwa masuala ya wanyama.

Bw Kariuki anasema kila mwaka yeye huzuru Lamu, ambapo husafiri kwa njia ya barabara ili kujionea wanyama na kuwapiga picha bure bilashi.

“Kuna mwaka nilisafiri kwa mara ya kwanza na kushuhudia wingi wa wanyamapori kandokando ya barabara. Tangu siku hiyo nikaamua kila ninapokuja Lamu nitumie usafiri wa barabara. Huniwezesha kuwaona wanyama wengi zaidi ya wale ninaoona nikiwa nimezuru mbuga nyingine za kitaifa nchini,” akasema Bw Kariuki.

Naye Sebastian White, mtalii wa kimataifa, anasema kuwepo kwa wanyamapori wengi Lamu ni afueni kwao kama watalii kwani wanapokosa au kupungukiwa na fedha za kuzuru mbugani kuona wanyama, wao hukimbilia kuja Lamu kujionea wanyama hao hao bila kizizi chochote.

“Kuna wakati ambapo tunakosa hela. Tunashindwa kukimu gharama ya kuzuru mbuga za kitaifa za wanyama. Hapo ndipo mimi binafsi hufikiria kuzuru Lamu. Hapa najua nitapiga picha na kujionea kila aina ya wanyama bila vizuizi,” akasema Bw White.

Wakazi aidha wana ombi kwamba wanyamapori wa Lamu wadhibitiwe ili kuepuka kuwaletea wapita njia madhara.

Bw Salim Ahmed alisema hajaisahau siku ambapo alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kasi na kisha ghafla binvuu akakutana na kundi la nyati waliokuwa wamejilaza katikati ya barabara eneo la Koreni.

“Karibu niwapiga nyati hao dafrao. Walikuwa wamejilaza katikati ya barabara bila ya kuwa na haraka au kushtuka. Ilinibidi niegeshe gari langu mahali, ambapo niliwasubiri hadi wakaondoka kwa hiari. Itakuwa bora endapo wanyamapori wetu watadhibitiwa ili wasihasiri madereva na abiria,” akasema Bw Ahmed.

Ikumbukwe kuwa ukwasi wa wanyamapori wapatikanao Lamu unachangiwa na kuwepo kwa misitu na miti mingi eneo hilo.

Lamu ni miongoni mwa kaunti chache za Kenya zenye asilimia kubwa ya misitu nchini.