Michezo

Safari ya Malkia Strikers kuelekea Uganda siku ya Ijumaa yatibuka, haijapata tiketi kutoka kwa wizara

May 17th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya voliboli ya wanawake ya Kenya almaarufu Malkia Strikers bado imekwama jijini Nairobi ikisubiri tiketi kutoka kwa Wizara ya Michezo kuelekea Uganda kwa michuano ya ukanda wa tano jinsi ilivyopangwa Ijumaa.

Taarifa kutoka kambi ya mabingwa hawa wa Afrika, ambao wamekutanishwa na Rwanda katika mechi ya ufunguzi itakayosakatwa Mei 19, hawajui kama watasafiri hadi jijini Kampala kwa kutumia ndege ama basi “kwa sababu bado wanasubiri wizara kuwapa tiketi”, ingawa wana matumaini ya kusafiri kesho (Jumamosi).  Mashindano haya yanafaa kutamtika Mei 25.

Wakati huo huo, mchujo wa Ukanda wa Tano wa wanaume utakaofanyika jijini Nairobi kutoka Juni 3-8 umevutia mataifa ya Kenya, Rwanda, Misri, Ethiopia, Tanzania, Uganda, Sudan na Sudan Kusini. Washindi wa Ukanda wa Tano wataingia mashindano ya All-African moja kwa moja. Mashindano hayo ya Afrika yataandaliwa mjini Rabat nchini Morocco kutoka Agosti 19-31, 2019.

Ratiba ya mchujo wa wanawake:

Mei 19

Ethiopia na Uganda

Kenya na Rwanda

 

Mei 20

Uganda na Rwanda

Ethiopia na Kenya

Mei 21

Kenya na Uganda

Rwanda na Ethiopia