Safari ya mgombeaji urais wa Roots kutoka Uganda hadi alipo sasa

Safari ya mgombeaji urais wa Roots kutoka Uganda hadi alipo sasa

NA WANDERI KAMAU

MWANIAJI urais George Wajackoyah alizaliwa mnamo Oktoba 24, 1959 katika Hospitali ya St Mary’s, jijini Jinja, nchini Uganda akiwa mwanawe marehemu Tito Olilo na Bi Melania Makokha.

Ijapokuwa alizaliwa nchini Uganda, yeye ni Mkenya, kwani wazazi wake walikuwa Wakenya.

Msomi huyo alikulia katika kijiji cha Indangalasia, Wanga Magharibi, eneo la Mumias, Kaunti ya Kakamega.

Kijiji hicho ndiko alikozaliwa babake na kulelewa.

Alipokuwa na umri wa miaka 16, Prof Wajackoyah alitoroka nyumbani kwao kwa kutumia lori hadi jijini Nairobi. Aliungana na watoto wengine wa mitaani, maarufu kama “chokoraa.”

Hata hivyo, aliokolewa na dhehebu la Kihindi la Hare Krishna, lililomchukua na kumpa makao. Alibadilisha dini yake na kujiunga na dhehebu hilo.

Ikizingatiwa alikuwa ashamaliza masomo yake katika shule ya msingi, alifadhiliwa kusoma katika shule ya upili na dhehebu hilo.

Alijiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya St Peter’s Mumias, alikomaliza masomo yake mnamo 1980.

Baada ya hapo alijiunga na Taasisi ya Mafunzo ya Polisi, Kiganjo, Kaunti ya Nyeri.

Hata hivyo, Prof Wajackoyah alitoroka nchini mnamo 1990 na kuelekea Uingereza.

Akiwa Uingereza, alijiunga na vyuo kadhaa, alikofanikiwa kupata shahada kadhaa za taaluma ya sheria.

Baadhi ya vyuo hivyo ni Wolverhampton, London, Warwick, Westminster na Birkbeck. Baadaye alielekea Amerika, ambako pia aliongeza masomo yake.

Ikizingatiwa wawaniaji urais wengine wameeleza msururu wa ahadi watakazotekelezea Wakenya ikiwa watachaguliwa kwenye uchaguzi wa Agosti, ahadi yake ya kuhalalisha matumizi ya bangi ndiyo imezua msisimko wa aina yake.

Licha ya ahadi hiyo kuonekana kama isiyo ya kawaida kwenye ulingo wa siasa nchini, kuna wanasiasa wengine duniani ambao washawahi kujizolea umaarufu kwa kutoa ahadi kama hizo.

Baadhi yao ni marehemu John Magufuli (Tanzania), Rodrigo Duterte (Ufilipino) na Donald Trump (Amerika).

Alipochaguliwa kama rais wa Tanzania mnamo 2015, Magufuli alijizolea umaarufu mkubwa kwa kuwafuta kazi au kuwachukulia hatua maafisa wa serikali mbele ya raia.

Duterte naye aliahidi kuwapiga risasi watu watakaopatikana kuwa walanguzi wa mihadarati, ahadi ambayo alitekeleza.

  • Tags

You can share this post!

Wajackoyah atikisa wagombea wakuu

Kapaito aanza kutesa wapinzani katika Ligi Kuu ya Ethiopia

T L