Michezo

Safari ya warembo wa St Marys Ndovea hadi fainali ya Chapa Dimba

April 1st, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

WASICHANA wa St Marys Ndovea ya Makueni waliibuka malkia wa Chapa Dimba na Safaricom Season Two katika Mkoa wa Mashariki na kujikatia tikiti ya kushiriki fainali za kitaifa baadaye mwaka huu.

St Mary Ndovea Secondary ambayo hunolewa na kocha, John Mutie ilitwaa tikiti hiyo ilipozoa mabao 2-1 mbele ya Chuka Starlets katika fainali iliyochezewa Kitui Show Ground mjini humo.

Kwenye nusu fainali St Mary Ndovea chini ya nahodha, Doris Wavinya iliikanyanga Sakuu Queens kwa mabao 3-0 na kufuzu kwa fainali. Nayo Chuka Starlets iliipepeta Karungwa Queens mabao 2-1.

Kocha huyo anadokeza kwamba wamepania kupiga kambi ya mwezi mmoja kushiriki mazoezi makali kujinolea fainali za kipute hicho zitakazopigwa mwezi Juni katika uwanja wa Kinoru Stadium mjini Meru katika Kaunti hiyo.

”Tunaratajia kupata shughuli zito katika fainali hizo ambapo lazima tujiandae vizuri kukabili wapinzani wetu,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa wamejaa furaha tele kufuzu kushiriki kipute hicho ikiwa ndiyo mwanzo kushiriki michuano hiyo na kubeba ubingwa wa Mkoa huo.

Aidha alisema hatua hiyo imewapa motisha wachezaji wake pia ilishangaza wengi waliokuwa wakiwadumisha na kusema kwamba hawangefika mbali kwenye mashidano hayo. Kadhalika alisema hawatakwenda kwa fainali hizo kama picha mbali watakwenda kushindana wakipania kutawazwa malkia wa kitaifa mwaka huu.

“Sina budi kushukuru wasichana wangu wote kwa kuonyesha mchezo mzuri pia ushirikiano mwema dimbani maana kama haingekuwa kujitolea kwao hawangefikia hadhi hiyo,” alisema na kuongeza kuwa analenga kuona wachezaji wake kadhaa wakiteuliwa katika kikosi cha kitaifa kutokana na michezo hiyo kitakachokwenda nchini Uhispania kushiriki mechi za kupimana nguvu na klabu tofauti katika taifa hilo.

Pia anashukuru wachezaji wake akiwamo Ruth Vaati, Daisy Chirchir, Naomi Mongina, Doris Wavinya na Hensley Nuru kwa kujitolea kwao maana mchango wao ulichangia ufanisi wao kwenye michuano hiyo.

Kocha huyo anashukuru wazazi na jamii ya eneo hilo kwa jumla kwa kuwaunga mkono kuanzia mwanzo hadi mwisho walipotawazwa washindi.

Alisema ufanisi wao ulichangiwa pakubwa na jinsi walivyokuwa wakishiriki mazoezi yao nyakati za asubuhi na jioni. Anatoa mwito kwa wachezaji wake kuonyesha haikuwa bahati walivyofuzu kwa fainali za kitaifa.

”Hata tukikosa kubeba ubingwa wa kitaifa itakuwa vyema kwa kikosi changu kushinda mechi kadhaa wakati wa fainali za kitaifa ili kuthibitisha haikuwa bahati kwa fainali za michezo ya mwaka huu,” alisema.

Kadhalika alidokeza kuwa anajaribu kutafuta jinsi atakavyowatuza wachezaji watakaoifungia timu hiyo mabao kwenye mechi za fainali. Mabingwa hao walituzwa kitita cha Sh200,000.

St Marys Ndovea secondary inajumuisha:

Mukii Mutuki, Venic Rabera, Violet Akoth, Ndanu Mutua, Catherine Kamanthe, Margaret Mutua, Catherine Wausi, Cecilia Mwende, Nyaleko Peter, Mary Kyalo, Rehema Mutie, Syliviah Meshack na Aminah Kimilu.