Habari Mseto

Safari za Madaraka Express kuongezeka

June 25th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Safari kwa reli ya kisasa (SGR) zitaongezeka kati ya Mombasa na Nairobi katika muda wa miezi mitano ijayo.

Safari za kila siku zitaongezeka zaidi ya 12 ambazo hufanyika kwa sasa kwa lengo la kuimarisha usafirishaji wa shehena za mizigo kati ya bandari ya Mombasa na depo ya kontena Embakasi, Nairobi.

Mwenyekiti wa kampuni inayojenga SGR China Communications Construction Company (CCCC) Lu Shan Ijumaa alisema kufikia Desemba 2018 safari hizo zitakuwa 28.

Kwa sasa, depo ya Embakasi ina uwezo wa kuchukua kontena 450,000 za urefu wa futi 20 kwa mwaka.

Kiwango chake cha awali kilikuwa kontena 180,000 za futi 20. Kwa siku hupokea magari manne ya moshi ambayo kila moja hubeba kontena 108.

Wasafirishaji wa bidhaa hulipa Sh35, 000 kwa kontena ya futi 20 na Sh40,000 kwa kontena ya futi 40 kati ya Mombasa na Embakasi.