Safari za Madaraka Express zaleta matumaini Pwani baada ya kiwingu cheusi cha Covid-19

Safari za Madaraka Express zaleta matumaini Pwani baada ya kiwingu cheusi cha Covid-19

Na CHARLES WASONGA

ILIKUWA ni furaha ya aina yake kwa abiria Jumatatu alasiri baada ya kuwasili katika kituo cha garimoshi cha Miritini, Mombasa kwa treni ya kwanza inayotumia reli ya kisasa ya SGR kutoka Nairobi.

Hii ni saa chache baada Shirika la Reli Nchini (KRC) kurejelea safari za treni hiyo, maarufu kama Madaraka Express baada ya serikali kuondoa marufuku ya watu kuingia na kuondoka Kaunti ya Nairobi na nyingine nne.

Huduma za uchukuzi wa abiria kwa treni hiyo zilisitishwa mnamo Machi 26, 2021, kama hatua mojawapo ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona baada ya kaunti za Nairobi, Kajiado, Machakos, Kiambu na Nakuru kuandikisha idadi kubwa ya maambukizi.

Lakini akihutubu wakati wa maadhimisho ya sherehe za mwaka 2020 za Leba Dei katika Ikulu ya Nairobi, Rais Uhuru Kenyatta alilegeza masharti hayo na kuondoa marufuku hayo.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba wenye hoteli na wafanyabiashara wengine wa Mombasa walifurahi kurejelewa kwa huduma za uchukuzi wa abiria kwa treni kutoka Nairobi hadi Mombasa.

Walisema hatua hiyo itafufua biashara katika sekta ya utalii na uchukuzi miongoni mwa sekta nyinginezo muhimu.

Janga la corona limeathiri pakubwa sekta za utalii na hoteli katika eneo zima la Pwani ya Kenya; hali iliyosababisha baadhi ya hoteli na vituo vya kitalii kupunguza idadi ya wafanyakazi au kufunga kabisa.

Nyingi za hoteli katika miji ya Mombasa, Kilifi, Malindi miongoni mwa mingine, ilipata hasara kubwa Aprili wakati serikali ilizima usafiri kutoka kaunti hizo tano za eneo la bara, ambazo huchangia wateja wao wengi.

Wahudumu wa teksi katika miji ya Pwani pia waliathirika na kufungwa kwa kaunti hizo tano.

Mnamo Jumapili, KRC lilitoa ratiba ya safari za treni zinazotumia SGR ambapo ile ambayo husimama kila kituo itakuwa ikiondoka Nairobi na Mombasa saa mbili za asubuhi. Treni ya moja kwa moja itakuwa ikiondoka Nairobi saa tisa za mchana na kuwasili Mombasa saa moja za jioni.

You can share this post!

Kane na Saka watawazwa Wachezaji Bora wa Mwaka 2021 katika...

Wawili wafariki, mmoja ajeruhiwa kwenye shambulio la...