Habari Mseto

Safaricom ilivyojiimarisha kifedha

May 5th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

FAIDA ya kampuni ya Safaricom baada ya kutozwa ushuru imeimarika kwa asilimia 14.7 hadi Sh63.4 bilioni.

Faida hiyo ilitokana na kuimarika kwa biashara ya matumizi ya M-Pesa na intaneti ya Safaricom.

Ni mwaka was aba mfululizo kwa Safaricom kupata faida. Faida hiyo ni ya mwaka wa kifedha uliokamilika Machi 2019.

Faida ya jumla ilikuwa ni Sh250.96 bilioni baada ya kukua kwa asilimia 7.1. Mkurugenzi Mkuu wa Safaricom Bob Collymore alipongeza kampuni hiyo kwa kupata faida hata baada ya kukabiliwa na mazingira magumu ya kibiashara.

“Tuliweza kupata faida kwa kulenga zaidi mteja, kuwekeza katika huduma bora, operesheni katika mfumo wetu na kuwapa wateja huduma tofauti,” alisema Bw Collymore.

Wakati huo, mapato kutokana na huduma yaliimarika kwa asilimia saba hadi Sh240.3 bilioni. Mapato ya M-Pesa yalikua kwa asilimia 19.2 hadi Sh74.99 bilioni huku mapato ya mali isiyobadilika yakiwa yameimarika kwa asilimia 22.7 hadi Sh8.19 bilioni.

Mapato kutokana na upigaji wa simu hayakukua sana. Yalikua kwa asilimia 0.3 pekee hadi Sh95.94 bilioni.

Mapato kutokana na matumizi ya intaneti yaliongezeka kwa asilimia 6.4 hadi Sh38.69. Hata hivyo, mapato kutokana na kutuma jumbe fupi yashuka kwa asilimia 1.3 bilioni hadi Sh17.5.

Kutokana na faida hiyo, bodi ya Safaricom ilipendekeza mgawo wa Sh0.62 kwa kila hisa, na itatoa jumla ya Sh24.84 bilioni kama mgawo kwa washikadau wake.