Habari za Kitaifa

Safaricom kutoa simu za bei nafuu

January 28th, 2024 1 min read

NA PATRICK ALUSHULA

KAMPUNI ya mawasiliano ya Safaricom imefichua kuwa simu za rununu inazozitengeneza huko Athi River zitakuwa nafuu kwa asilimia 30 kuliko zinazoagizwa kutoka nje.

Mkurugenzi mkuu wa Safaricom, Peter Ndegwa, alisema bei hiyo itasaidia kampuni hiyo kuongeza matumizi ya simu, zinazotumia mtandao wa 4G na kukuza mapato kutokana na biashara ya data.

“Matarajio yetu si kupata kiasi kikubwa cha pesa kwenye kifaa, lakini ni kunufaisha wateja nchini na kuongeza mapato kupitia biashara yetu iliyopo,” alisema Bw Ndegwa.

Kiwanda hicho cha simu cha East Africa Device Assembly Kenya Limited kilianza kufanya kazi Oktoba 2023 na kinaendeshwa kama muungano, kati Safaricom, TeleOne, na Jamii Telkom.

Kiwanda hicho kinaweza kutengeneza simu milioni tatu kwa mwaka, na kuwa na nafasi ya kuongezeka zaidi kulingana na mahitaji.

Bw Ndegwa alisema kiwanda hicho pia kinalenga kusafirisha simu hizo ukanda wa Afrika Mashariki na pia kupanua uzalishaji zaidi, hadi kwenye vifaa vingine vinavyotumia data.