Habari

Safaricom yaadhimisha miaka 19 ikiwa na habari njema kwa wateja

October 23rd, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Safaricom imewaletea wateja fursa ya kununua vifurushi visivyo na muda wa ukomo vya data, kupiga simu, na kutuma ujumbe mfupi ikiadhimisha miaka 19 tangu kuanza shughuli zake nchini Kenya.

Hatua hii inakuja mnamo wakati kukiwa na kesi mahakamani ambapo wakili Adrian Kamotho aliishtaki kampuni hiyo pamoja na Airtel Kenya kwa kuweka muda wa vifurushi kupoteza thamani.

Chini ya mpango huu mpya unaoanza kutekelezwa mara moja, zaidi ya wateja 33 milioni wa Safaricom wanayo fursa ya kununua vifurushi vya data na muda wa kupiga simu kuanzia kiwango chochote cha shilingi moja na kupanda.

“Kama pendekezo la kudumu, wateja wanaonunua mipango ya kupiga simu na kutuma SMS kwa kubonyeza *544# watapata asilimia 50 ya muda wa ziada kuongea kila wanapofanya hivyo ili wapate fursa ya kuongea zaidi kwa gharama nafuu,” amesema Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Michael Joseph.