Habari

Safaricom yapata faida ya Sh35.65 bilioni kipindi cha miezi sita

November 1st, 2019 1 min read

Na BRIAN NGUGI

KAMPUNI ya Safaricom imepata faida ya Sh35.65 bilioni baada ya mapato ya M-Pesa na data kipindi cha miezi sita hadi kufikia Septemba 2019 kuongezeka kwa asilimia 14.4 licha ya mapato kutokana na kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi (SMS) kudidimia.

Huu ni mwaka wa nane sasa ikiendelea kupata faida baada ya kuondoa makato mengine ikiwemo ushuru.

Katika kipindi cha miezi sita, mapato kutokana na M-pesa yalikuwa kwa asilimia 18.2 na kufikia Sh41.97 bilioni nayo ya vifurushi vya data ya Intaneti kuongezeka kwa asilimia nne hadi kuwa Sh19.78 bilioni.

Mapato kutokana na huduma za wateja ama kupiga simu au kupokea ambayo huwa tegemeo kuu la kampuni hiyo yalipungua kwa asilimia 1.4 na kuwa Sh46.87 bilioni nayo yale ya huduma za ujumbe mfupi yalipungua kwa asilimia 11 na kuwa Sh8.6 bilioni.

“Ukuaji wa mapato kipindi cha nusu-mwaka hadi Septemba ulikuwa wa asilimia 5.3 uliochochewa zaidi na huduma za M-Pesa na data pamoja na ukuaji wa wateja na hivyo kusawazisha sehemu za mapato kuporomoka ambazo awali zilikuwa ni tegemeo,” amesema Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom anayeondoka Michael Joseph akitangaza ripoti hiyo ya kampuni katika makao makuu jijini Nairobi.