Habari Mseto

SafeBoda yarejesha huduma zake nchini

January 24th, 2024 1 min read

NA BRIAN AMBANI

KAMPUNI ya kutoa huduma za pikipiki kwa njia ya mtandao, SafeBoda, inalenga kurejelea huduma zake nchini Kenya, miaka mitatu baada ya kusitisha shughuli zake nchini.

“Tumerudi!”, kampuni hiyo ikasema katika akaunti yake ya mtandao wa X.

“SafeBoda inarejea Nairobi,” kampuni hiyo ilisema katika wavuti wake Jumatatu huku ikisema itazindua upya shughuli zake baada ya siku 13.

Kampuni hiyo ilisitisha shughuli zake nchini Kenya mnamo Novemba 2020 wakati wa janga la Covid-19 ili kuangazia zaidi shughuli zake nchini Uganda.

Kampuni hiyo ilikuwa imepata hasara baada ya janga hilo kudhibiti shughuli za uchukuzi kufuatia kafyu iliyowekwa na serikali.

“Ingawa shughuli kiuchumi Nairobi zinafufuka kutoka pigo la Covid-19, uchukuzi umeathiriwa zaidi. Hii ina maana kuwa biashara yetu haiwezi kunawiri katika mazingira haya na kwa bahati mbaya haijulikani ni lini uchumi utarejelea hali yake ya kawaida,” SafeBoda ilisema wakati huo (2020).

Hadi kufikia wakati huo ilipofunga biashara zake Kenya, SafeBoda ilikuwa imeweka kandarasi na zaidi ya wahudumu 1.8 milioni wa boda boda nchini.