Habari MsetoSiasa

Sahau uwaziri mkuu, Karua amwambia Uhuru

November 21st, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua amemwambia Rais Uhuru Kenyatta asahau kupata nafasi ya uwaziri mkuu amalizapo kipindi chake mwaka wa 2022.

Bi Karua alisema kuwa hata kama katiba ya sasa itafanyiwa mageuzi, Rais Kenyatta hawezi kuwa waziri mkuu ikizingatiwa kuwa amehudumu kwa kipindi cha mihula miwili akiwa rais.

“Namwambia ndugu yangu Uhuru Kenyatta kufutilia mbali mawazo ya kuwa Waziri Mkuu, kwani kikatiba haikubaliki. Hilo halikubaliki hata ikiwa tutaifanyia katiba ya sasa mageuzi. Namwambia hivyo kama mtu anayemuunga mkono na atakayeendelea kumuunga mkono,” akasema Bi Karua akihutubu jijini Nairobi.

Kauli yake inajiri baada ya Rais Kenyatta kusema kwamba hatajali kuhudumu kama waziri mkuu baada ya muhula wake kukamilika mnamo 2022.

Kumekuwa na wasiwasi kuhusu lengo halisi la ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) ambalo lilibuniwa na Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga, huku baadhi ya viongozi wakidai ni njama fiche ya viongozi hao kujitengenezea nyadhifa baada ya 2022.

Kwenye mkutano maalum wa viongozi mbalimbali wa Mlima Kenya katika Ikulu ya Sagana wiki iliyopita, Rais Kenyatta alisema kuwa yuko tayari kuhudumu katika nafasi yoyote kwa “manufaa ya Wakenya.”

“Sijui lolote kuhusu yaliyopo kwenye ripoti ya BBI, ingawa ninasikia watu wakidai kuwa Uhuru Kenyatta anataka kuwa waziri mkuu wa Kenya. Sitajali kuwa katika uongozi nikishikilia nafasi kama hiyo. Hata hivyo, tunapaswa kuyashughulikia masuala muhimu kwanza,” akasema Bw Kenyatta.

Baadhi ya wakereketwa pia wamekuwa wakidai kwamba Rais Kenyatta ni mchanga sana kung’atuka uongozini. Miongoni mwao ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi (COTU) Bw Francis Atwoli.

“Mnataka Uhuru aende wapi? Hataenda mahali popote kwani angali mchanga,” akasema Bw Atwoli. Hofu kuhusu lengo halisi la ripoti hiyo inatokana na kucheleweshwa kutolewa kwake licha ya jopo hilo kutangaza limemaliza kuiandaa na iko tayari kuiwasilisha kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Kwenye mkutano wa Sagana, Rais Kenyatta alikosolewa vikali kwa kulishinikiza eneo la Mlima Kenya kuunga mkono BBI, badala ya kuangazia changamoto kuu za kiuchumi zinazowakabili wakazi.