Sahib asherehekea ‘bathdei’ kwa kutawala Autocross Nanyuki, Hamza abwaga babake Asad

Sahib asherehekea ‘bathdei’ kwa kutawala Autocross Nanyuki, Hamza abwaga babake Asad

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA mtetezi Sahib Omar alisherehekea kugonga umri wa miaka 35 kwa kushinda duru ya saba ya mashindano ya KCB Nanyuki Autocross katika eneo la Batian View, Jumapili.

Sahib tayari alinusia ushindi baada ya mpinzani wake mkuu Eric Bengi kushindwa kufikia muda wake katika mashindano ya kufuzu kushiriki fainali.Ushindi wa Sahib katika eneo la Nanyuki ulikuwa wa tatu msimu huu baada ya kutawala duru mbili katika eneo la Jamhuri Park jijini Nairobi.

Dereva huyo kutoka timu ya Ray Racing alivuna ushindi katika eneo la Batian akiendesha gari la Subaru Impreza GC8.

Alilemea Bengi katika mzunguko wa kwanza kwa sekunde 0.003. Sahib alishinda mzunguko wa pili sekunde mbili mbele ya Bengi kabla ya kumzidia maarifa tena kwa sekunde 0.005 katika mzunguko wa tatu.

Isitoshe, Sahib alizoa alama mbili za nyongeza kwa kuweka kasi ya juu ya siku (FTD) katika mzunguko wa pili alioumaliza kwa dakika 1:54.72.

Qahir Rahim apiga kona katika barabara zilizojaa matope katika eneo la Batian View mjini Nanyuki…PICHA/GEOFFREY ANENE

“Ninahisi vizuri sana kutwaa taji la Nanyuki katika siku yangu ya kuzaliwa nikisherehekea kufikisha miaka 35. Barabara zilikuwa telezi saa za asubuhi, lakini zilikauka baadaye mashindano yakiendelea. Kwa jumla, barabara hizi ni nzuri sana kupaisha magari,” alisema Sahib.

Kiongozi wa kitengo cha magari ya 4WD, Lovejyot Singh alizidiwa ujanja katika juhudi zake za kukamata nafasi mbili za kwanza baada ya gari lake kukumbwa na hitilafu.Naye, Yuvraj Rajput aliibuka mshindi katika kitengo cha Bambino kwa kumpiku mfalme wa raundi ya sita Karanveer Singh Rooprai.

Hamza Anwar alitawala kitengo cha wazi akimaliza mbele ya baba yake Asad Anwar.Kitengo cha Bambino kilikuwa na pacha John na Joline Jessel. Wawili hawa ni wajukuu wa bingwa wa kitengo cha magari cha Rally Raid mwaka 2010 Sammy Jessel.

Sam Karangatha aliandikisha ushindi wake wa tatu msimu huu katiia kitengo cha 2WD Non-Turbo akimzima hasimu wake Rajveer Thethy.

  • Tags

You can share this post!

Corona: Serikali yahimizwa kufungua uchumi

Mshirika wa karibu wa Shahbal ahamia UDA