Michezo

Sajili wapya kuisaidia KCB kutamba voliboli 2019

December 14th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA wa voliboli barani Afrika mwaka 2006, KCB wametambulisha rasmi sajili wake wapya huku wakilenga kuanza maandalizi ya mwaka 2019 hapo Desemba 17, 2018.

Wachezaji wapya ni Leonida Kasaya, Noel Murambi, Violet Makuto, Christine Njambi, Veronica Kilabat, Jemima Siangu na Truphosa Chepkemei. Wametambulishwa kwa wanahabari katika makao makuu ya benki ya KCB katika jumba la Kencom katikati mwa jiji la Nairobi.

Mlezi wa klabu hiyo, ambayo imeshinda mataji tisa ya Afrika Mashariki na Kati, Judith Sidi Odhiambo amefurahia kukaribisha wachezaji hao wapya akisema, “Kama benki tunalenga kuwa na msimu mzuri na kikosi chote cha KCB.”

Kocha mpya wa KCB, Japheth Munala, ambaye pia amekuwa akifunza timu ya taifa almaarufu Malkia Strikers, ameongeza kwamba wachezaji hao wapya wataipiga jeki KCB na pia kumpa kikosi kikubwa cha kuchagua timu thabiti.

“Kikosi cha sasa cha KCB ni thabiti kuliko kikosi kingine chochote nchini Kenya katika safu ya ulinzi. Wachezaji hawa watafanya kikosi kiwe kamilifu katika uzuiaji wa mipira na kutuma makombora,” amesema Munala, ambaye amerejea KCB kutoka Kenya Pipeline aliyoiongoza kushinda ligi mwaka 2014, 2015, 2016 na 2017.

Pipeline ilimaliza katika nafasi ya tatu mwaka 2018 nyuma ya washindi Kenya Prisons na nambari mbili KCB. Munala alinoa KCB kati ya mwaka 2008 hadi 2013.