Michezo

Saka kuwa kizibo cha Sancho kambini mwa Dortmund

April 27th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BORUSSIA Dortmund wamefichua azma ya kumfanya chipukizi matata wa Arsenal, Bukayo Saka kuwa kizibo cha Jadon Sancho anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kujiunga na Manchester United mwishoni mwa msimu huu.

Akijivunia jumla ya mabao 17 na kuchangia mengine 19 hadi kufikia sasa muhula huu, Sancho amekuwa kivutio kikubwa kambini mwa vikosi mbalimbali katika soka ya bara Ulaya.

Mbali na Man-United ambao wako radhi kuweka mezani kima cha Sh17 bilioni kwa minajili ya Sancho, klabu nyinginezo zinazokeshea huduma za kiungo huyo mzawa wa Uingereza ni Liverpool, Juventus, Real Madrid na Bayern Munich.

Iwapo Dortmund watashawishika kumwachilia Sancho, kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kimeweka Saka kileleni mwa orodha ya wanasoka watakaorithi nafasi yake.

Haya ni kwa mujibu wa magazeti ya Mirror na The Sun.

Ingawa kwa sasa anachezeshwa kama beki wa kushoto kambini mwa Arsenal, Saka mwenye umri wa miaka 18, hutamba sana anapowajibishwa kama kiungo mvamizi.

Alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal mwaka jana chini ya mkufunzi Unai Emery katika kivumbi cha Europa League.

Baada ya kuridhisha zaidi katika kibarua chake cha kwanza, alipata uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Arsenal baada ya mabeki Kieran Tierney na Sead Kolasinac kupata majeraha ya muda mrefu.

Hadi msimu huu wa kivumbi cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ulipositishwa kwa muda mwanzoni mwa Machi 2020, Saka alikuwa amewafungia Arsenal mabao matatu na kuchangia mengine manane katika mashindano yote.

Ingawa ni matamanio ya kocha Mikel Arteta kuendelea kujivunia maarifa ya Saka uwanjani Emirates, huenda ikamwia vigumu kumdhibiti chipukizi huyo ambaye gazeti la The Sun limesisitiza kwamba atakuwa radhi kupokea mamilioni ya Dortmund badala ya Sh420,000 pekee ambazo kwa sasa analipwa na Arsenal kwa wiki.

Kufikia sasa, Saka angali na mwaka mmoja pekee katika kandarasi yake na Arsenal ambao wameanza kumvizia chipukizi Jude Bellingham, 16, wa Birmingham kuwa kizibo cha Saka.