Habari za Kaunti

Sakaja aagiza pombe ya makali kuondolewa kwa steji za matatu

February 24th, 2024 1 min read

NA HILLARY KIMUYU

GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja amemwagiza Afisa Mkuu wa Usalama katika Kaunti Tony Kimani, kuhakikisha kwamba maduka yote yanayouza pombe ya makali almaarufu ‘wines and spirits’ yanaondolewa karibu na steji za mabasi na matatu kwa muda wa siku saba zijazo.

Bw Sakaja alitoa kauli hiyo Ijumaa baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA), kuhusu iddi ya watu waliofariki kutokana na ajali katika barabara za jiji la Nairobi.

Kwenye mkutano aliouongoza, ulioujumuisha uongozi wa Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) na maafisa wa NTSA, Bw Sakaja alielezea wasiwasi wake kutokana na idadi kubwa ya watu ambao wamekuwa wakifariki barabarani kutokana na matumizi ya vileo.

“Hatutaruhusu hali ya kutozingatiwa kwa sheria za trafiki kuendelea jijini. Nairobi ni jiji kuu la taifa hili.  Tunafanya kila tuwezalo kulainisha hali. Leo (Ijumaa) nimeagiza kutolewa kwa maduka yote ya pombe ya makali yaliyo karibu na steji za matatu,” akasema.

Kulingana na Bw Sakaja, madereva na manamba huwa wanakunywa vileo katika maduka hayo, wanapowangoja abiria kuingia katika magari yao.

“Tumewapoteza wapendwa wetu kutokana na kutozingatiwa kwa kanuni za barabarani kwa sababu ya ulevi,” akasema.