Habari za Kaunti

Sakaja motoni kwa ‘kusahau’ wakazi jijini

February 11th, 2024 2 min read

NA VINCENT ODUOR

GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja amejipata matatani huku baadhi ya viongozi wakidai ametoroka kuwajibikia wakazi jijini na kumakinikia safari za ng’ambo ambazo hazina faida.

Bw Sakaja hakuwepo wakati ambapo mlipuko wa gesi ulitokea Mradi, Embakasi Mashariki na kusababisha mauti ya watu sita majuma mawili yaliyopita huku wengine zaidi ya 300 wakijeruhiwa vibaya.

Wakati huo alikuwa kwenye ziara Afrika Kusini na aliporejea siku tano baadaye, mambo yalikuwa yashaharibika.

Inadaiwa baadhi ya maafisa wake walimfeli kabisa katika kushughulikia janga hilo.

Siku moja baada ya tukio, Naibu wake Njoroge Muchiri alifika eneo la janga angalau kuthibitisha uongozi wa kaunti ulikuwa pamoja na waathiriwa.

Siku mbili kabla ya mlipuko, kulikuwa na kisa kingine cha moto eneo la Juakali katika barabara ya Landhies. Vibanda vya kibiashara vilichomeka katika kisa hicho na Bw Sakaja hakuwepo.

Aidha utendakazi wa Bw Sakaja nao umewekwa kwa mizani huku wakazi wa jiji wakiendelea kukosa maji. Barabara zinaendelea kuwa mbovu, mfumo wa ukusanyaji takataka umesambaratika, mitaro ya kupitisha majitaka imezibika huku pia kukiwa na mfumo usioeleweka wa ukusanyaji mapato.

“Nairobi ni kati ya kaunti ambazo zinatumia hela nyingi zaidi katika safari za nje na ndani ya nchi. Binafsi sijaona manufaa ya ziara hizo kwa sababu huwa Bw Sakaja haziweki wazi na kama Seneta siwezi kufahamu yaliyoafikiwa,” akasema Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.

Baada ya mlipuko wa gesi kutokea Embakasi, shughuli za kuwasaidia walioathirika zilikuwa zikiongozwa na serikali kuu, mbunge wa eneo hilo Babu Owino, Bw Sifuna na Shirika la Msalaba Mwekundu.

Diwani wa Kileleleshwa Robert Alai, alidai kuwa uongozi wa Kaunti ya Nairobi upo mikokoni mwa serikali kuu na Bw Sakaja ni gavana ambaye hana ushawishi wowote.

Bw Sakaja hata hivyo, ametetea ziara zake akisema zimesaidia kuleta fedha na wawekezaji katika kaunti.

“Nilipata euro 1.4 milioni (Sh245 milioni) kutoka jijini Paris kupiga jeki mpango wa lishe shuleni katika kaunti ya Nairobi. Je, wajua kuwa mimi ni naibu mwenyekiti wa muungano wa miji 40 (C40) kuhusu vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi chini ya uenyekiti wa Meya wa jiji la London, hadhi ambayo imeifaidi Nairobi?” gavana Sakaja akauliza.

Alipuuzilia mbali madai kuwa yeye ni mateka wa Ikulu na hana usemi kupitia mfumo wa ukusanyaji ushuru.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Gitile Naituli, amewalaumu raia wanaowachagua viongozi kwa kutowafuatilia na kuwaweka kwenye mizani.

“Wale ambao wamechaguliwa wanaendelea kuunda pesa. Kuenda ziara za nje kunaandamana na marupurupu tele ya kusafiri ndiposa baadhi yao hawapendi kuonekana kwenye kaunti,” akasema Prof Naituli, mtaalamu wa masuala ya usimamizi na uongozi.

“Kuna baadhi ya viongozi ambao hata wakati ambapo hawapo nje ya nchi huwezi kuwapata wakishughulikia changamoto za watu ambao wanawawakilisha katika kaunti zao,” akaongeza.

Mtangulizi wa Bw Sakaja, Bw Mike Sonko, alifahamika sana kwa kujitokeza maeneo mbalimbali jijini Nairobi hasa wakati ambapo wakazi walikuwa wakisaka msaada.

Bw Sonko mara nyingi alikuwa akikutana na raia na hata aliunda kundi la ‘Sonko Rescue Team’ kusaidia wakazi wakati wa majanga.